Sunday, September 23, 2012

FISI WALA WATU WAIBUKA GETA






MATUKIO ya watoto kuuawa kwa kuliwa na fisi yameibuka tena mkoani Geita, baada ya mtoto Hawa Baltazari (5) kukamatwa na kuliwa na fisi katika Kijiji cha Nyakato kata ya Nyanguku.

Vitendo vya watoto kuliwa na fisi katika Mkoa na Wilaya ya Geita yaliibuka katika kipindi cha Januari 2011 hadi Februari 2012, ambapo watoto 12 waliuawa kwa kuliwa na fisi katika maeneo ya Nyijundu, Busolwa, Kharumwa, Kamena huku baadhi ya wananchi wakiyahusisha matukio hayo na imani za kishirikina.

Ilielezwa kwamba tukio wiki iliyopita lilitokea wakati  mtoto huyo akitoka kujisaidia umbali wa mita 50 kutoka nyumba ya bibi yake aitwaye Mariamu Bwegera (65) ambaye alikuwa akiishi na mtoto huyo enzi za uhai wake.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paul alisema tukio hilo lilitokea saa 1:30 usiku wa kuamkia  Alhamisi iliyopita  ambapo mtoto huyo wakati anakamatwa na fisi alikuwa na dada yake,Grace Sadick(17) ambaye alikuwa amemsindikiza kwenda kujisaidia chooni.



Alifafanua kuwa wakati wanatoka chooni ghafla alitokea fisi na kumkamata Hawa na kuondoka naye huku akipiga mayowe na dada yake kuomba msaada wa kumwokoa mikononi mwa fisi,mayowe ambayo hayakusaidia kunusuru uhai wa mtoto huyo.

Kamanda Paul,alisema baada ya tukio hilo wananchi walikusanyikana na kuanza kumtafuta mtoto huyo ambapo mwili wake ulikutwa vichakani umbali wa mita 500 kutoka nyumbani kwao ukiwa umeliwa sehemu za kichwani,shingoni na mguu wa kulia.

Aidha aliongeza kuwa jitihada za kumsaka fisi huyo zinafanyika kwa kushirikiana na idara ya wanyama pori wilaya ili kumkamata na kumuua.

No comments:

Post a Comment