Thursday, September 20, 2012

CHADEMA WAGOMA MWALIKO WA TEDWA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekataa mwaliko wa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, kushiriki katika semina aliyoiandaa kuhusu amani na usalama wa nchi.

Chama hicho kimesema hakitashiriki katika semina hiyo wakati huu kwa kuwa kinasubiria hatua za Rais kuhusu mauaji ya kisiasa yaliyotokea katika mikoa mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Chadema, John Mnyika, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema chama hicho kimechukua hatua hiyo kikitambua umuhimu wa amani na usalama wa nchi na wajibu wa Jeshi la Polisi pamoja na Vyama vya Siasa katika kukuza demokrasia ya vyama vingi.

Mnyika alisema hatua hiyo imefikiwa kufuatia utendaji dhaifu na wa kipropaganda unaoonyeshwa na Tendwa uliosababisha Kamati Kuu ya Chadema kumtangaza kuwa ni adui wa demokrasia na hafai kuwa katika nafasi aliyo nayo.

“Kamati Kuu iliazimia kuwa pamoja na kuendelea kuheshimu sheria ya vyama vya siasa, Chadema haitashiriki shughuli zozote zitakazosimamiwa na John Tendwa hadi hapo atakapoondolewa katika nafasi yake na kuteuliwa msajili mwingine,” alisema.

Alisema Kamati Kuu ya Chadema ilifanya kikao maalumu Septemba 9 mwaka huu kilichojadili hali ya siasa nchini kufuatia mfululizo wa mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi katika shughuli za kisiasa za Chadema na mipango ya baadhi ya viongozi wa Serikali ya kudhibiti Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa mbinu haramu.

“Katika majadiliano ya kina kabla ya kufikia maamuzi Kamati Kuu pamoja na mambo mengine ilieleza kusikitishwa na kauli za kisiasa ambazo zimekuwa zikitolewa na Tendwa, zenye mwelekeo wa kukibeba Chama Cha Mapinduzi ( CCM) na serikali,” alisema.

Hivi karibuni, Tendwa alitoa kauli kwamba atavifuta vyama vya siasa ambavyo shughuli zake zitasababisha mauaji.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment