NAPE AKIKARIBISHWA NA NAIBU WAZIRI -9778
Naibu waziri Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi. Anastazia James Wambura (kushoto) akimkaribisha Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo katika ofisi za wizara hiyo leo jijini Dar es Salaam.
NAPE AKIKARIBISHWA NA LILI BELEKO 9798
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi Lilian Beleko (kulia) akimkaribisha kwa furaha Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye wizarani hapo leo hii jijini Dar es Salaam.
NAPE AKIONGEA NA WAANDISHI -9893
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akiongea na waandishi wa Habari leo katika ofisi za wizara hiyo kwa mara ya kwanza toke ateuliwe kuwa Waziri.Mhe Nape amehaidi kuleta maendeleo kupitia wizara hiyo kwa hali na mali.
NAPE NA MSHANA-9980
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye (kushoto) akiongea na menejimenti ya shirika la Utangazaji Tanzania-TBC (hawapo pichani) wakati alipotembelea makao makuu ya shirika hilo ili kujua changamoto walizonazo na jinsi gani atawasaidia kama waziri mwenye dhamana.
Na Rabi Hume, Modewjiblog
Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ameripoti kwa mara ya kwanza katika ofisi yake ya wizara hiyo akiambatana Naibu wake, Mhe. Anastasia Wambura na kupokelewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Prof. Elisante Ole Gabriel kisha kufanya kikao na watumishi wa wizara kwa kutoa vipaumbele vyake katika utendaji wa kazi.
Mhe. Nape alivitaja vipaumbele vya wizara yake kuwa itakuwa ni kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na watu wa ndani na nje ya ofisi, wasiogopane, heshima baina ua watumishi wa wizara na watu wa nje na uwazi baina yao hata kama atakuwa amefanya kosa yeye.
Alisema kuwa katika uongozi wake wa wizara hiyo hatopenda kuona wadhifa wake unakuwa chanzo cha wafanyakazi kumuogopa na kushindwa kusema ukweli hali ya kuwa kuna tatizo na kama kutakuwa na watu wa aina hiyo basi hataweza kufanya nao kazi.
“Mimi nataka utumishi uwe mbele kuliko utukufu wa cheo kama nimefanya makosa niambieni ili tuweze kuboresha utendaji wa kazi wa ofisi yetu na niweke wazi sitaweza kufanya kazi na mtu anaeogopa kusema ukweli, kuweni huru kabisa kufanya kazi na tusiogopane kwenye ukweli tuseme,” alisema Mhe. Nape.
Aidha alisema kuwa wizara hiyo ni ofisi ambayo inaonyesha taswira ya serikali kutokana na kuhusika na habari na kama wafanya kazi wa wizara watashindwa kufanya kazi kwa kasi ambayo wanahitajika kwenda nayo basi hawatakuwa wakiitendea haki serikali kwa kutokutimiza wajibu wao.
Aliongeza kuwa rais Dkt. John Pombe Magufuli ana mipango ambayo ameipanga kuifanya kwa wizara hiyo na utendaji wao wa kazi ndiyo ambao utafanikisha kufanyika na kukamilika kwa mipango hiyo ikiwepo mipango ya kuisaidia timu ya taifa (Taifa Stars) kufika mbali kisoka ikiwezekana kucheza kombe la dunia.
“Tufanye kazi pamoja kuisaidia serikali na hii ndiyo wizara inaweza kuonyesha hali ya serikali jinsi ilivyo na natambua wazi kuwa rais wetu ana malengo na wizara hii na sisi tusimwangushe,” aliongeza Mhe. Nape.
Pia alizungumzia kuhusu michezo na kuahidi kushirikiana na vyama vinavyohusika na michezo na hata yeye amekuwa mtu wa michezo hivyo anatambua changamoto walizonazo na watafanya kazi kwa ushirikiano ili kupeleka mbele gurudumu la michezo nchini.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel alimshukuru waziri kwa kuonyesha kuwa na nia ya dhati kufanya kazi kwa kasi ya rais na kwa niaba ya watumishi wenzake wa wizara hiyo akamuahidi kwamba watafanya nae kazi kwa ushirikiano kama jinsi anavyohitaji wizara hiyo ifanye kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya waziri huyo.