Umbali
wa takribani kilomita moja kutoka ofisini kwake Ikulu jijini Dar es
Salaam, Rais Dk.John Magufuli anatembea hadi Wizara ya Fedha anapowakuta
‘wazembe’ wakiwa nje ya ofisi.
Tukio hilo la jana lilikuwa la kushtukiza, lisilotarajiwa na wakazi
wa jijini kumuona Rais Magufuli akiwa katika siku ya pili ya utawala
wake, ‘akikatiza’ kwa mguu kwenda wizarani hapo.
Akiwa katika kampeni na baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha
urais, Rais Magufuli aliwaonya watumishi wa umma kuacha kufanya kazi kwa
mazoea na uzembe na wasioweza mabadiliko, waanze kuondoka.
Akiwa katika kuthibitisha kauli mbiu yake ya ‘hapa ni kazi tu’,
Rais Magufuli aliingia wizarani hapo na kukuta baadhi ya viti sita
vikiwa wazi, taarifa ikaeleza kwamba watumishi wahusika walikuwa nje ya
ofisi kunywa chai.
Ili kupata ushahidi usiotiliwa shaka, Rais Magufuli alishika kiti
kimoja baada ya kingine, akiuliza jina la mtumishi anayekitumia na
mahali alipo.
Ziara hiyo aliifanywa muda mfupi baada ya kumuapisha Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, George Masaju aliyemteua katika siku ya kwanza ya
utawala wake.
Tukio hilo ambalo lilikuwa ni la aina yake liliwashangaza baadhi ya wananchi na kujikuta wakimshangilia kila alipopita.
Alipofika katika wizara hiyo alianza kuingia ofisi moja baada ya
nyingine huku akihoji baadhi ya wafanyakazi ambao hawakuwepo wakati huo
wa kazi.
“Hiki kiti ni cha nani, amekwenda wapi… na nayekalia kiti kile yule
anaitwa nani… ina maana hawa wote sita hawapo wameenda wapi wakati
wewe ni bosi wao au wameenda kunywa chai… haya ,” alihoji Rais
Magufuli.
Aliwata watendaji wakuu wa wizara hiyo kutekeleza majukumu yao
kikamilifu kwa kukusanya kodi hasa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa
ambao wanadaiwa kuikwepa.
Alitoa rai kama hiyo kwa Mamlaka ya Kodi (TRA) akitaka watii na kufuata sheria katika utendaji kazi wao.
Rais Magufuli alisema katika serikali yake hakuna kiongozi yeyote
serikalini atakayetoa ‘memo’ kwa TRA kusamehe ulipaji wa kodi halali za
serikali.
Alisema kodi inaiwezesha serikali kutoa huduma za kijamii kama
elimu ya bure kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kuanzia mwakani.
Aidha, aliagiza kampuni zinazotangaza kufilisika kutoa taarifa
sahihi serikalini kuhusu ulipaji kodi za serikali ulivyofanywa na
mhusika.
POSHO KWA WABUNGE
Rais Magufuli alipiga marufu malipo ya posho kwa wabunge yanayofanywa nje ya zile wanazolipwa na Bunge.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment