WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amewahakikisha wahandisi kwamba
endapo atachaguliwa kuwa Rais wa serikali ya Awamu ya Tano hatawaangusha
na atahakikisha anawatumia vyema kwa ajili ya kujenga uchumi kutoka wa
chini kwenda wa kati.
Dk Magufuli ambaye pia ni mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM) aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akifunga maadhimisho ya
Siku ya Wahandisi Tanzania 2015 yaliyowashirikisha wahandisi kutoka
ndani na nje ya nchi.
“Nawahakikishia wahandisi Mungu akijaalia kule mbele siwezi
kuwaangusha, siku za nyuma nilikuwa naagizwa ila sasa nitakuwa naagiza
mimi, hivyo msiwe na wasiwasi na maamuzi nitakayoagiza na kufanya
yatakuwa kwa faida ya wahandisi na Watanzania wote,” alisema.
Alisema amekuwa serikalini miaka 15 na amekuwa wizara ya ujenzi na
katika miaka hiyo maisha yake yamekuwa na uhusiano mkubwa na wahandisi
na amejifunza mengi kupitia wao na ni sekta ambayo anatambua manufaa
yake na changamoto zake, hivyo hataweza kuwaacha.
“Duniani popote sehemu iliyofanikiwa ni sehemu ambayo palikuwa na
wahandisi na wametumiwa vizuri, hivyo nami nitahakikisha nawatumia sana
katika kujenga uchumi na tunataka kuhakikisha sekta ya maji na viwanda
inakuwa,” alisema.
Aidha alisema endapo akichaguliwa ataanzisha mamlaka katika
halmashauri itakayohusu masuala ya wahandisi kama ilivyo Tanroads ili
kuwawezesha kupata bajeti yao watakayoisimamia wenyewe bila kuingiliwa
na wanasiasa.
Aliongeza kuwa, “pamoja na kwamba sijaja kuwaomba kura ila ni vyema
mkamchagua mtu anayewafahamu wahandisi vizuri maana hatawaangusha…
lakini naomba niwaombe kura msije mkasema sikuwaomba, naombeni kura
zenu”.
Aliwakemea baadhi ya wahandisi ambao wamekuwa wakiharibu sifa ya
wahandisi kwa kufanya kazi chini ya kiwango na kuwataka kubadilika na
kufanya kazi kwa weledi ili kuendelea kujenga sifa nzuri na kupata kazi
nyingi zaidi.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Nyamuhanga alisema
tangu mwaka 2005-2015 ujenzi wa barabara umeimarika ambapo barabara
nyingi zimejengwa na zingine zipo katika hatua mbalimbali.
Alisema katika kipindi hicho wamejenga madaraja makubwa 12 na
yamekamilika pamoja na madogo 7,200 na mengine saba yanaendelea kujengwa
likiwemo la Kigamboni na Kilombero.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Profesa Ninatubu Lema
alisema wamejipanga kuendelea kulitumikia taifa ili ifikapo 2025 waweze
kujivunia kulitoa taifa kutoka uchumi wa chini kwenda wa kati.
No comments:
Post a Comment