Sunday, June 14, 2015

MAKAMBA AHIDI KUMNG`OA SUGU

Kada wa CCM, aliyetangaza nia ya kugombea urais, January Makamba ameahidi kumng'oa Mbunge wa Mbeya mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Mbilinyi (Sugu) katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Makamba alitoa ahadi hiyo jana alipozungumza na wanachama wa CCM, jijini hapa alipokuwa akiomba wamdhamini ili aweze kugombea urais kupitia (CCM).


Aliwaambia wanachama hao kwamba Sugu hana hadhi ya kuongoza jiji kubwa kama la Mbeya na kwamba ikiwa CCM kitampitisha kugombea urais ataweka kambi jimboni hapo ili kukipa ushindi chama chake.


Sugu alishinda kiti cha ubunge Mbeya mjini mwaka 2010, kupitia Chadema.


Makamba alisema, endapo atapata ridhaa ya  kupeperusha bendera ya CCM, atahakikisha anavunja makundi ndani ya chama kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu, mwaka huu.


Aliongeza kuwa ikiwa chama kitaingia katika uchaguzi mkuu huku kukiwa na makundi, itakuwa vigumu kufanya vizuri na kwamba majimbo mengi yalichukuliwa na upinzani mwaka 2010 kutokana na chuki miongoni mwa wanaCCM.


Aidha, Makamba aliahidi kukijenga upya chama ili kiweze kupendwa na makundi yote katika jamii huku akisema kwamba atahakikisha anapambana na usaliti unaofanywa na baadhi ya wanachama wa CCM.


"Mimi nikipewa ridhaa ya kugombea urais nitamaliza suala la usaliti miongoni mwa wanachama na hili nitalifanya haraka ili kukijenga chama," alisema.


Aliwaambia wanachama hao kwamba siasa za kutukanana na kutoleana kashfa zimepitwa na wakati kwa kuwa wagombea wote wanatoka CCM.


Alifananisha kitendo cha wagombea kutoleana kashfa halafu mmoja wapo akapitishwa kugombea urais ni sawa na mtu kulamba matapishi yake.


Aliwaambia wanachama hao kwamba yeye akipitishwa kugombea urais, atahakikisha chama kinakuwa salama na kukubalika na kada zote katika jamii.


Makamba aliahidi kuwasaidia vijana kupata ajira kwa kuweka mazingira mazuri yakiwamo ya kufufua viwanda pamoja na kujenga vipya.


Aliongeza kuwa wananchi wa mkoa wa Mbeya hawatajutia uamuzi wao kwa kumuunga mkono katika safari ndefu ya kuelekea kuijenga Tanzania mpya.


Wanachama wa CCM 1678 kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Mbeya walijitokeza kumdhamini Makamba ili kutimiza masharti aliyowekwa na chama kabla ya kuingia katika mchujo wa wagombea.


Mpaka jana Makamba alikuwa amezunguka kuomba udhamini katika mikoa mitano ya Dodoma, Iringa, Njombe, Songea na Mbeya na kupata wadhamini zaidi ya 7000.

No comments:

Post a Comment