AMA kweli Simba imepania msimu ujao kwani imetangaza rasmi
kumrejesha kikosini mchezaji wake kutoka Kenya, Raphael Kiongera, baada
ya kuridhika na hali yake ya kiafya pamoja na uwezo wa uwanjani
alioonyesha akiwa na KCB inayoshiriki Ligi Kuu Kenya (KPL).
Kiongera aliyepelekwa KCB kwa mkopo, ameshapona
majeraha lake la goti na tayari ameanza kuonyesha makeke yake katika
ligi hiyo ya Kenya akiwa amefunga mabao matatu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia
Hanspope, alisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia maendeleo
ya Kiongera hasa kwenye suala lake la afya na kwamba wameridhishwa na
sasa wameamua kumrejesha Simba kwa ajili ya Ligi msimu ujao.
“Kiongera ni mchezaji halali wa Simba,
tumejiridhisha kwamba amepona vizuri na ana uwezo mzuri wa kupambana
uwanjani, hivyo tunatarajia kuwa atarejea na kujiunga na wenzake ifikapo
kipindi cha maandalizi ya Ligi,” alisema Hanspope.
Kiongera aliumia goti la mguu wa kulia katika
mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliomalizika dhidi ya Coastal Union
kwenye Uwanja wa Taifa Septemba 21, 2014 na kulazimika kukaa nje ya
uwanja kwa zaidi ya miezi minne.
Kurejeshwa kwa mchezaji huyo kunafanya idadi ya
wachezaji wa kigeni kwa Simba kuwa wanne na kusaliwa na nafasi moja
ambayo inayowaniwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit
Mavugo.
No comments:
Post a Comment