Mashambulizi ya angani yanayoongozwa na muungano wa Saudi Arabia
yamelenga maeneo ya waasi wa kishia wa Houthi ndani na katika maeneo
mengine kusini mwa mji wa Aden.
Hatua hii imetokea baada ya kumalizika hapo jana usiku kwa muda wa
usitishaji mapigano uliolenga kutoa nafasi ya kufikisha misaada ya kwa
waathirika wa mgogoro huo.
Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Waziri wa mambo ya nchi za
nje wa Yemen amesema muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umeamua
kutoendeleza kipindi cha kusitisha mapigano kwa sababu makubaliano ya
awali yalikiukwa mara kadhaa na waasi wa Houthi.
"Hicho ndicho tulichokisema awali – kwamba wakianza tena tutaanza tena,"
alisema Reyad Yassin Abdullah anayetokea upande wa serikali ya Yemen
iliyoko uhamishoni mjini Riyadh nchini Saudi Arabia. Ameongeza kuwa
muungano huo hautarajii kuwa na makubaliano yoyote mapya ya kusitisha
mapigano.
Hata hivyo waasi wa Houthi hawakupatikana mara moja kutoa maoni yao juu ya hilo.
Mabomu ya angani yalidondoshwa katika ikulu ya rais inayoshikiliwa na
waasi mjini Aden, na dhidi ya makundi ya wanamgambo Magharibi na
Mashariki mwa mji huo na pia kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa ambako
waasi wa Kihouthi na wapiganaji wamekuwa wakipambana. Hii ni kulingana
na wakaazi wa maeneo hayo. Bado hapajakuwa na habari zaidi juu ya
majeruhi wa mkasa huo.
Kwa zaidi ya wiki sita, Saudi Arabia na washirika wake wa Kisunni
wamekuwa wakiwashambulia waasi wa jamii ya Houthi na vikosi vya
wanajeshi watiifu kwa rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.
Muungano huo unasema waasi hao wanaungwa mkono na taifa la Waislamu wa
Kishia la Iran.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran azungumzia hali ilivyo Yemen
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Mohammed Javad
Zariff ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua jukumu zaidi nchini Yemen
ikiwemo kuingia ndani ya Yemen kuhakikisha misaada ya kiutu inasambazwa.
"Bila shaka Umoja wa Mataifa unaweza kuchunguza na kuhakikisha misaada
inayopelekwa kwa watu wa yemen, ni misaada ya kiutu, ni muhimu pia
kupeleka msaada wa matibabu kwa wagonjwa na waliojeruhiwa, kwahivyo
tunazihitaji jitihada za jamii ya kimataifa ili kuishughulikia Yemen,"
alisema waziri Zariff.
Makubaliano ya siku tano ya kusitisha mapigano yalioanza usiku
wa Jumanne yalisimamisha mashambulizi ya angani na kutoa nafasi ya
misaada ya kiutu katika nchi hiyo iliozingirwa, lakini wakaazi wa maeneo
ya kusini mwa Yemen kama Shabwa, Dhalea na Abyan wamesema mapigano
makali ya ardhini yaliendelea licha ya makubaliano hayo.
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry
amesema nchi yake inaunga mkono hatua ya kuendeleza makubaliano ya
kusitisha mapigano lakini ujanja unaofanywa na waasi wa Houthi unaifanya
hatua hiyo kuwa ngumu kutekelezwa. Aidha mjumbe mpya wa Umoja wa
Mataifa anayeshughulikia mzozo wa Yemen Isamil Ould Cheikh Ahmed ametoa
wito wa makubaliano ya kusitisha mapigano kurefushwa
No comments:
Post a Comment