Rais Jakaya Kikwete amemteua Anthony Peter Mavunde kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, kuanzia jana.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uhamisho wa wakuu 10 wa wilaya kwa nia
ya kuongeza ufanisi katika uongozi wa Wilaya mbali mbali nchini.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilieleza kuwa,
katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete amemhamisha Luteni Edward Ole Lenga
kutoka Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida kwenda kuwa mkuu wa wilaya
mpya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera. Luteni Lenga anachukua nafasi iliyoachwa
wazi na Luteni Kanali Benedict Kulikela Kitenga ambaye alifariki dunia
Aprili 20, mwaka huu, 2015.
Wakuu wengine wa wilaya waliohamishwa ni Elizabeth Chalamila Mkwasa
kutoka Wilaya ya Dodoma kwenda Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro; Dkt
Jasmine Tisike kutoka Wilaya ya Mpwapwa kwenda Wilaya ya Dodoma; Agnes
Elias Hokororo kutoka Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma kwenda Wilaya
ya Tunduru, mkoani humo humo na Fadhili Nkurlu kutoka Wilaya ya Misenyi,
Mkoa wa Kagera kwenda Wilaya ya Mkalama.
Wengine ni Chande Bakari Nalicho kutoka Wilaya ya Tunduru kwenda
Wilaya ya Namtumbo; Festo Shem Kiswaga kutoka Wilaya ya Mvomero kwenda
Misenyi; Darry Ibrahim Rwegasira kutoka Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa
Kagera kwenda Wilaya ya Biharamulo, mkoani humo humo; Elias Choro John
Tarimo kutoka Wilaya ya Biharamulo kwenda Chunya, Mkoa wa Mbeya na
Deodatus Lukas Kinawiro kutoka Wilaya ya Chunya kwenda Wilaya ya
Karagwe, Mkoa wa Kagera.
No comments:
Post a Comment