Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuanguka ghafla akiwa kwenye
foleni ya kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura
kwa teknolojia mpya ya Biometric Voters Registratio
n (BVR).
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi saa 6:30 mchana kwenye
kituo cha Lusyoto, kata ya Mpuguso katika eneo la Ushirika, wilayani
Rungwe, ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza uandikishaji wa wapigakura
wilayani humo.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo wamemtaja aliyepoteza
maisha kwenye tukio hilo kuwa ni Mary Kabejela anayekadiriwa kuwa na
umri wa miaka 60, mkazi wa Ushirika wilayani Rungwe.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya mashuhuda walisema Mary akiwa
kwenye mstari wa foleni ya kuelekea kwenye chumba cha uandikishaji,
ghafla alionyesha kudhoofika na kuishiwa nguvu na kisha kudondoka chini.
Amani Mwaipaya, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema baada ya
mama huyo kuanguka, wananchi walimwinua na kumpeleka Hospitali ya Wilaya
ya Rungwe ya Makandana, ambako alipoteza maisha wakati akipatiwa
matibabu.
“Tulimwona akianza kulegea na ghafla akaanguka chini, ndipo
tulipomwinua na kumpakia kwenye gari tukampeleka hospitali, lakini
wakati daktari akianza kumhudumia alifariki dunia,” alisema Mwaipaya.
Baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa waliozungumzia tukio
hilo, walisema kifo cha mama huyo huwenda pia kimechangiwa na kusimama
kwenye foleni kwa muda mrefu kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahamed Msangi, hakupatikana
kuthibitisha tukio hilo licha ya simu yake ya mkononi kuita kwa muda
mrefu.
Mwandishi wa habari hizi alifika kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mbeya na kuelezwa kuwa Kamanda Msangi amesafiri kikazi na kwamba
kaimu wake, Nyigesa Wankyo pia alikuwa nje ya ofisi kikazi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya
Mbeya Mjini, David Mwambigija, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako,
ambaye yupo wilayani Rungwe kama wakala wa chama chake kwenye kazi hiyo,
alisema uandikishaji unafanyika kwa kasi ndogo, hali inayosababisha
watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu na hata kusababisha presha
kuwapanda.
“Inawezekana huyu mama akawa amekufa kutokana na presha kupanda,
kwani alisimama kwenye foleni tangu asubuhi huku akipigwa na jua kali,
kutokana na umri wake kuwa mkubwa huenda presha ilimpanda na kumpelekea
kupoteza maisha,” alisema Mwambigija.
Alisema kasi ya uandikishaji siyo nzuri kutokana na watumishi wa
serikali waliopewa kazi hiyo kuonekana kama wanajifunza hivyo kutumia
muda mrefu kukamilisha kumwandikisha mtu mmoja, hali inayosababisha watu
kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu.
Mbali na tukio hilo la kifo, zoezi la uandikishaji wapigakura
kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura lilianza juzi kwa kusuasua
wilayani Rungwe kutokana na madai kwamba mtandao ulikuwa na matatizo.
Kufuatia mtandao kuwa siyo mzuri, idadi kubwa ya vituo vya
kuandikishia wapigakura vilichelewa kuanza uandikishaji hadi saa 4:00
asubuhi hali ilipoanza kutengemaa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Veronica Kessy,
alikiri kuwapo kwa changamoto katika siku ya kwanza ya uandikishaji,
ikiwamo tatizo la mtandao kusumbua.
Alisema hata hivyo tatizo hilo lilikuwa la muda mfupi na baadaye
hali ilikuwa nzuri na kasi ya uandikishaji ikaendelea vizuri kama
lilivyopangwa katika maeneo mengi.
Kessy alisema ni vituo vichache tu ambavyo zoezi la uandikishwaji
wapigakura liliingia dosari kwa kukumbwa na changamoto ndogondogo kama
vile kuchelewa kufunguliwa, kujitokeza kwa idadi kubwa ya wananchi
kuliko uwezo wa waandikishaji na tatizo la mtandao kusuasua.
Katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya zoezi la uandikishwaji lilianza
juzi katika kata 10 zilizopo ndani ya Bonde la Uyole, ambako
liliendelea vizuri licha ya wananchi kulalamikia kasi ndogo ya
waandikishaji.
Katika kituo cha Isyesye kulitaka kutokea tafrani baada ya wananchi
kumshtukia mtu mmoja anayedaiwa kuwa kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kukaa pembeni mwa kituo cha kuandikishia wapiga kura akiwa na
daftari na kalamu akiorodhesha watu wanaojiandikisha.
Wananchi hao walimjia juu mtu huyo wakitaka kumpiga kabla ya askari
wa Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumwondoa kwenye eneo hilo kabla
hajaanza kushushiwa kipigo.
Awamu ya tatu ya uandikishaji katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura ilianza jana mkoani Dodoma na Tabora utaanza leo, huku Katavi
ukiwa umeanza tangu Jumatatu iliyopita.
Awamu ya kwanza ilihusisha mkoa wa Njombe ambayo ulikamilika
katikati ya Aprili, wakati awamu ya pili inaendelea katika mikoa ya
Ruvuma, Iringa, Lindi na Mtwara.

No comments:
Post a Comment