WAKATI polisi wakiendelea kukalia jalada la Mbunge wa Urambo
Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), anayetuhumiwa kubaka na kutishia
kuua binti wa miaka 16, sasa suala hilo limefikishwa katika ubalozi wa
Marekani.
Mbali na hatua hiyo, binti huyo pia amelifikisha jambo hilo kwa
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amiri
Manento akitaka msaada zaidi.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumatano, binti huyo na dada yake,
walisema wameamua kuomba hifadhi katika ubalozi wa Marekani kwa madai ya
kuhofia usalama wao kutokana na vitisho wanavyozidi kuvipata kila
kukicha.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, binti huyo alisema wamefikia
hatua hiyo baada ya kuona polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
(DDP), hawataki kulifikisha suala lao mahakamani wanakoamini haki yao
itapatikana.
Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakisikia kuwa Marekani ni vinara wa
utawala bora na demokrasia, hivyo aliamua kwenda ubalozi wa nchi hiyo
hapa nchini wasaidiwe.
“Kapuya inaonekana anatisha au analindwa sana, lakini sisi tutahakikisha haki yetu tunaipata kwa njia zozote,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa serikali imeshindwa kuwapa hifadhi kutokana na
vitisho wanavyovipata, na wanahofia kuuawa hali inayowafanya wawe
waangalifu zaidi.
Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa mabinti hao walikwenda
ubalozi wa Uingereza kuomba hifadhi hiyo ambako walielekezwa kuwa
wakienda katika ubalozi wa Marekani shida yao itatatuliwa.
Mmoja wa mabinti hao alithibitisha kwenda katika balozi hizo ambako waliamini wangepata hifadhi waliyoihitaji.
“Tulienda ubalozi wa Uingereza tukaambiwa tuende ubalozi wa Marekani
ndio tungeweza kupewa hifadhi, lakini tulipoenda tuliambiwa tupeleke
barua kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani au kutoka Tume ya Haki za Binadamu
na Utawala Bora ndipo tupokelewe,” alisema.
Tanzania Daima Jumatano liliwasiliana na ofisa mmoja wa ubalozi wa
Marekani ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, ambaye alikiri
suala hilo kulisikia katika viunga vya ofisi zao.
“Huyo binti mmoja alikuja hapa, lakini baada ya kubanwa na walinzi
alishindwa kujieleza fresh… wakamwambia Marekani haihusiki na hilo tukio
hivyo hawana msaada kwao.
“Si kweli kuwa ubalozi wa Marekani tulimuambia akalete barua hizo anazozisema ili tumpe hifadhi,” alisema.
Alibainisha kuwa suala hilo halikufikishwa kiofisi.
Katika hatua nyingine, mtoto huyo amelalamikia mashirika yasiyo ya
kiserikali kwa kuwatelekeza licha ya mwanzoni kuwaahidi kushirikiana
nao.
Alisema sasa mashirika hayo yanaonekana kuogopa vitisho vinavyotolewa na Kapuya.
Binti huyo alisema anakusudia kushirikiana na jamaa, ndugu na
marafiki kufanya maandamano hadi mlangoni katika ofisi ya Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Alisema lengo la maandamano hayo ni kutaka kujua kwanini waziri huyo na polisi wanamlinda Kapuya katika tuhuma hii.
Tanzania Daima Jumatano, lilimtafuta Waziri Nchimbi, kuhusu
malalamiko hayo, lakini simu yake ilikuwa ikiita muda mrefu pasi majibu
na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu.
Manento ashauri
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, Jaji mstaafu
Amiri Manento, alikiri kulisikia jambo hilo kwa muda mrefu, lakini hajui
kwanini halijafikishwa mahakamani.
Jaji Manento alibainisha kuwa jambo hilo lipo wazi kwakuwa pande hizo
mbili zipo, hivyo ni kazi ya polisi na Mwendesha Mashitaka (DPP)
kulifikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Aliongeza kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, haiwezi
kuchunguza suala hilo kwakuwa binti anayelalamikiwa kufanyiwa vitendo
hivyo yupo na mlalamikiwa wake (Profesa Kapuya) yupo, hivyo mamlaka
zinazohusika zifanye kazi yake.
Akizungumzia hatua wanazopaswa kuchukua kuhusu suala hilo, Jaji
Manento alisema malalamiko hupelekwa kwa tume, kisha inachunguza na
kumpa ushauri anayehusika.
“Sisi hatuna mahusiano na ubalozi wala hatuwezi kuandika barua
kushauri ubalozi upokee watu, hayo ni mambo ya ndani ya nchi, ambayo
mabalozi hawapaswi kuyaingilia.
“Tunachoshauri sasa kwa kuwa suala la kubaka ni suala la jinai, na
kama aliyebakwa anaona kuwa Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mwendesha
Mashitaka hawataki kumshitaki Kapuya, basi watafute waendesha mashitaka
binafsi kesi ifunguliwe mahakamani moja kwa moja bila kutegemea uamuzi
wa mwendesha mashtaka (DPP) wa kukubali au kukataa suala hilo lifikishwe
mahakamani.
“Kwa utaratibu huo, mtuhumiwa atafika mahakamani, na waliomlalamikia
watatoa ushahidi, hata kama katika hatua hii mwendesha mashitaka anaweza
kuifuta kesi mahakamani kwa ‘nole’ watu watakuwa wameshajua kama
serikali inalinda wahalifu au la,” alisema.
Polisi wazungumza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alipoulizwa
juu ya hatua waliyofikia katika kupeleka kesi hiyo mahakamani, alisema
bado wanaendelea na uchunguzi.
Alipoulizwa ni uchunguzi wa namna gani wanaoufanya na kama
wameshapata maelezo ya Profesa Kapuya, Kamanda Wambura alisema miongoni
mwa hatua za uchunguzi ni pamoja na kumuhoji mtu anayetuhumiwa.

No comments:
Post a Comment