WAKAZI wa Kigamboni, wilayani Temeke, wamemtaka Rais Jakaya
Kikwete kuacha kuwaamini watendaji wake kuwa suala lao la kupinga
kuondoka katika eneo hilo kupisha ujenzi wa mji wa kibiashara
limekwisha.
Wakizugumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye viwanja vya Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kifurukwe, Kata ya
Kibada, Dar es Salaam juzi, wakazi hao zaidi ya 300 walisema hawako
tayari kuondoka eneo hilo kwa gharama yoyote ile.
Walisema suala hilo la kupisha ujenzi mpya wa Jiji la Kigamboni
halijakwisha kutokana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kuliendesha
kinyume cha sheria na propaganda.
Mwenyekiti wa mkutano huo, Issaya Mathayo, alisema wakazi hao hawana
nia ya kumwaga damu bali wanaitaka serikali kuwa makini ili kuepuka
kuufikisha mgogoro huo katika hatua hiyo.
“Mnajua suala la ardhi si la mchezo mchezo, kuitoa ni rahisi lakini
kuipata tena gharama yake ni kubwa, hivyo tunaahidi hakuna
atakayeondolewa kirahisi…kikubwa sheria zitumike,”alisema Mathayo.
Alisema sheria zikifuatwa hakuna atakayeondolewa kwa kuwa kila ardhi
inapobadilishwa matumizi kwa ajili ya mandeleo, serikali hutumia sheria
zake za mipango miji kwa kuwapanga wananchi katika eneo husika na si
kuwaondoa.
“Kinachofanyika hapa ni ujanja hata hizo fomu ambazo tunaletewa
tuzijaze zinaonekana si za kiserikali, kwani hazina hata nembo ya taifa
hali inayotutia mashaka,” alisema.
Alisema hakuna mchakato wa kueleweka wa tathmini za mali zao
uliofanyika kwa ajili ya fidia, hivyo wameamua kuiacha kamati iliyoundwa
kwa ajili ya kusimamia masilahi yao kutokana na kuwa upande wa
serikali.
Mwalami Mwinyimvua, alisema tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 2008
ieleweke kuwa hakujawa na makubaliano yoyote kati ya serikali na
wananchi hao, kinachoendelea ni propaganda katika vyombo vya habari vya
serikali.
Aliwalaumu madiwani wa Jimbo la Kigamboni kushindwa kuwatetea wakazi
hao katika kujua hatima yao na badala yake wamejiingiza kwenye kazi ya
udalali wa viwanja kwa masilahi binafsi.
Aliongeza kuwa hadi sasa wanaiheshimu kazi kubwa inayofanywa na Mbunge
wao, Faustine Ndugulile, ya kupigania haki zao na kuahidi kuwa
hawatamuacha kokote atakakokwenda.
No comments:
Post a Comment