Saturday, May 18, 2013

WABUNGE WAMJIA JUU JK

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo wamepania kutoa madukuduku yao wakati wa mkutano wao na Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete, mjini Dodoma.
Katika mkutano huo ulioitishwa na Rais Kikwete mwenyewe, baadhi ya wabunge wamepania kumwambia ukweli kuhusiana na udhaifu wa serikali na mawaziri wake ambao walidai unakipa nguvu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mbunge mmoja mwenye kawaida ya kuishambulia serikali, aliliambia gazeti hili kuwa atamwambia ukweli Rais Kikwete jinsi alivyo dhaifu katika kukabili chokochoko za kidini ambazo katika siku za hivi karibuni zimeanza kuliathiri taifa.
“Nikipata nafasi nitamwambia ukweli Rais Kikwete kwamba udhaifu wake katika kufanya maamuzi magumu, unaipa umaarufu CHADEMA, umesababisha chokochoko za kidini kuongezeka, mawaziri na watendaji wake wengine ni mafisadi, CCM anayoiongoza imezidi kupasuka na upole wa Waziri Mkuu, Pinda umeifanya serikali ionekane dhaifu,” alisema.
Kwa mujibu wa mbunge huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, amepania pia kuzungumzia jinsi Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba alivyoipaisha CHADEMA kwa kuunda njama ambazo leo zimeanza kuonekana kuwa ni za uongo.
Rais Kikwete ambaye amewasili mjini Dodoma tangu jana, leo anatarajiwa kuanza mkutano wake wa siku mbili na wabunge wa CCM ambapo pamoja na mambo mengine, kujadili mwenendo wa wabunge wa chama hicho katika mjadala wa bajeti wa wizara mbalimbali.
Ingawa CCM haijaweka hadharani ajenda za mkutano huo, lakini duru za siasa ndani ya chama hicho zililiambia gazeti hili kuwa Rais Kikwete pamoja na mambo mengine anatarajiwa kuzungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM, hali ya kisiasa nchini na ndani ya chama hicho tawala, na msimamo wa wabunge wa CCM katika mijadala ya Bunge la bajeti inayoendelea mjini Dodoma.
Mambo mengine yanayotarajiwa kuibuka katika mkutano huo ni hali ya usalama nchini, hasa kutokana na matukio ya hivi karibuni ya mashambulizi ya kigaidi na jinsi serikali inavyoshindwa kukabiliana na matukio hayo.
Habari kutoka kwa baadhi ya wabunge wa chama hicho mjini Dodoma, zilisema hoja ya misimamo tofauti ya wabunge CCM katika kujadili bajeti, inaweza kutawala mkutano huo kutokana na mwenendo wa baadhi yao kuamua kuikosoa serikali na wakati mwingine kutishia kutoiunga mkono bajeti.
Baadhi ya wabunge ambao hata katika vikao vya ndani vya chama hicho wamekuwa wakishambuliwa kwa misimamo yao ya kuipinga serikali ni pamoja na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, Kange Ligola (Mwibara), Luaga Mpina (Kisesa), Ally Kessy (Nkasi) na Nimrod Mkono (Musoma Vijijini).
Katika vikao hivyo ambavyo hufanyika chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, wabunge hao wamekuwa wakionywa na kutakiwa kuacha kuishambulia serikali, lakini hawajakoma kufanya hivyo kwa madai kuwa wanawawakilisha waliowachagua.
Katika kikao cha hivi karibuni cha wabunge wa CCM, Ligola na Filikunjombe walishambuliwa na baadhi ya wabunge na mawaziri wakihoji endapo wabunge hao wapo kambi ya upinzani au la.
Kauli ya hivi karibuni ya Lugola kwamba baadhi ya mawaziri wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, imemweka pabaya mbunge huyo.
Hoja hiyo ambayo ilishazimwa na Spika wa Bunge, Anna Makinda, inatarajiwa kuibuka tena leo mbele ya Rais Kikwete hasa baada ya juzi Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika kipindi cha maswali na majibu kumtaka mbunge huyo ataje majina ya mawaziri aliodai wanauza unga.

No comments:

Post a Comment