Rais wa TFF, Leodegar Tenga
MKUTANO Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unatarajiwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu baada ya ule wa Dharura wa marekebisho ya Katiba uliopangwa kufanyika Julai 13, mwaka huu.
Tarehe hizo zimepangwa na kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika leo (Mei 9 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais wake Leodegar Tenga ambacho kupokea rasmi maagizo ya Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA) na kupanga utekelezaji wake.
“Kamati ya Utendaji ya TFF imepokea rasmi barua ya FIFA na kupanga utekelezaji wake. Tumepokea maagizo ya FIFA yanayotuelekeza cha kufanya, si TFF wala mtu mwingine yeyote anayeweza kuongeza jambo lingine.
“Maagizo ni undeni Kamati ya Maadili, Kamati ya Rufani ya Maadili, fanyeni marekebisho ya Katiba, anzeni tena uchaguzi, waliokuwepo na wengine wapya waruhusiwe. Tumejitahidi kuhakikisha uchaguzi uwe kabla ya Oktoba 30 mwaka huu kama FIFA walivyotuagiza,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na waandishi wa habari leo.
Amesema kazi kubwa itakuwa ni kutayarisha kanuni hizo, kwani Kamati za Maadili lazima ziwe na kanuni zake na kuhakikisha kuwa hakuna mgongano kati ya Kanuni za Nidhamu na Kanuni za Maadili.
Pia Rais Tenga amesema kuna kazi ya kuangalia jinsi zitakavyoingia katika uchaguzi ambapo maana yake muda wa mchakato wa uchaguzi utakuwa zaidi ya siku 40 za sasa, hivyo mabadiliko hayo yatagusa vilevile Kanuni za Uchaguzi.
Kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji, rasmu ya mwanzo ya Kanuni hizo inatakiwa iwe imetoka kufikia Mei 30 mwaka huu ambapo itapelekwa FIFA kwa ajili ya kupata mawazo yao kabla ya kuendelea na hatua inayofuata.
Juni 15 mwaka huu Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana kupokea mapendekezo hayo ambapo baada ya kuyapitisha itayapeleka tena FIFA. Taarifa (notice) ya Mkutano Mkuu wa Dharura ambayo kikatiba ni siku 30 itatolewa Juni 12 au 13 mwaka huu.
Baada ya Mkutano Mkuu wa Dharura wa marekebisho ya Katiba, Kamati ya Utendaji itakutana kati ya Julai 14 na 15 mwaka huu kuunda Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Maadili ili kuruhusu mchakato wa uchaguzi uanze.
No comments:
Post a Comment