Wednesday, May 1, 2013

MWENYEKITI WA BAVICHA AZIPIGA NA MKEWE

MWENYEKITI wa Baraza la Vijana (BAVICHA) la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, Nestory Mashishanga, anashikiliwa na polisi akidaiwa kumjeruhi mkewe kwa kisu kutokana na wivu wa kimapenzi.


Mashishanga anadaiwa kutenda tukio hilo Aprili 20, mwaka huu, katika mji wa Rulenge saa tano usiku baada ya kumkuta mkewe akiwa jirani na baa ya Upendo kwa dada yake kisha kuanza kumshambulia kwa kisu kwenye pafu la kulia na sehemu ya bega la kushoto.

Kaimu mganga mkuu wa Hospitali ya Rulenge, Dk. Prosper Malya, alikiri kupokelewa kwa mgonjwa huyo akisema kuwa alishonwa sehemu iliyojeruhiwa ingawa hali ilibadilika kesho yake baada ya kushindwa kupumua.

Dk. Malya aliongeza kuwa katika kufanya zaidi uchunguzi walikuta damu imevimbia ndani ya pafu lililopatwa na jeraha na kulazimika kumfanyia upasuaji ili kuona kama damu hiyo inaweza kutoka.

Akielezea tukio hilo, majeruhi huyo, Neema Nassib (24), ambaye amelazwa wodi namba tano, alisema kuwa alikuwa mtaa wa Upendo kumsaidia dada yake shughuli mbalimbali ambapo alikutwa na mumewe saa 12 jioni.

Alisema kuwa mumewe alikaa hapo hadi nyakati za kulala ndipo alipoanzisha fujo za kutaka arudi naye kwake kitongoji cha Murutambikwa kijiji hicho cha Rulenge.

Alisema kuwa kwa kuwa hawakuwa na maelewano ndani ya nyumba na ni siku nyingi ameshindwa kuishi naye kwa ustaarabu alimkatalia na ndipo alianza kumshambulia huku akitoa kisu na kuanza kumchoma sehemu mbalimbali za mwili wake.

Aidha alidai kuwa katika kuangushana na kupiga kelele alikuja dada yake na shemeji yake pamoja na mfanyakazi wa baa kuingilia kati vurugu zao na hatimaye kumuokoa na kumkimbiza hospitalini kwa lengo la kupata matibabu.

Alisema kabla ya tukio hilo, wamekuwa na vurugu za kila mara kuhusu kutoaminiana katika ndoa kila mmoja akimtuhumu mwenzake lakini mumewe amekuwa akijulikana kwa kukutwa na wake aliozaa nao.

Wanandoa hao walioana wakati Neema akiwa kidato cha tatu na kuacha shule huku kijana huyo akiwa anafanya kazi katika mgodi wa Kabanga Nikeli kama mlinzi.

Alisema kuwa hivi karibuni Mashishanga aliacha kazi mgodini na kujiunga na siasa katika chama cha CHADEMA wilayani Ngara na kuchaguliwa mwenyekiti BAVICHA.

No comments:

Post a Comment