Mawakili wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare, anayetuhumiwa kwa makosa ya ugaidi, jana waliwasilisha maombi ya kutaka Mahakama Kuu ifute mashitaka ya pili aliyofunguliwa mteja wao baada yale ya kwanza kufutwa kwa madai kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ametumia vibaya madaraka yake.
Maombi hayo yaliwasilishwa jana Mahakama Kuu na jopo la mawakili linalomtetea Lwakatare, akiwamo Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu na kudai kwamba haikuwa halali DPP kufuta kesi ya awali iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18, mwaka huu na kisha muda mfupi kuirudisha.
Lissu na jopo la mawakili katika maombi yao kwa Jaji wa Mahakama Kuu, Lawrance Kaduri, wanadai kwamba, mamlaka aliyonayo DPP katika kufuta mashitaka na muda mfupi kuyarudisha ni ikiwa ataona anataka kutenda haki, kulinda maslahi ya umma pamoja na kuzuia matumizi mabaya ya mahakama. Alisema DPP ingawa sheria inamruhusu kufuta mashitaka, lakini katika kesi ya Lwakatare alikiuka Sheria namba 6 ya kuendesha mashitaka ya mwaka 2008.
Wakili mwingine, Mabere Marando, aliingia rasmi jana kumtetea Lwakatare.
Kesi hiyo dhidi ya Lwakatare, ilifunguliwa katika Mahakama ya Kisutu Machi 18, mwaka huu na muda mfupi baadaye DPP akaifuta na siku hiyo hiyo alifunguliwa kesi nyingine ya mashitaka yanayofanana na yale ya awali lakini mbele ya hakimu mwingine.
Lissu alidai kuwa ibara ya 59 ya Katiba ya nchi inasema ili mkutano wa kupanga ugaidi uwe na sifa za kuitwa hivyo, ni lazima uhusishe zaidi ya watu watatu na kwamba katika kesi inayomkabili Lwakatare, anayeshtakiwa ni mtu mmoja tu, hivyo hauwezi kuitwa ugaidi.
Upande wa mashitaka ukiwasilisha hoja zake, ulidai kuwa kesi inayomkabili Lwakatare ilifutwa kutokana na kukosewa na kufunguliwa katika jalada la mahakama za chini badala ya za juu hivyo isingefaa kuendelea.
Aidha, upande huo ulidai kuwa maombi ya Lwakatare siyo muda mwafaka kwa kuwa bado uchunguzi wa kesi unaendelea na kwamba mashitaka yanayoweza kubadilishwa ama kufutwa kwa kuwa sheria haijatoa tafsiri kuhusu ugaidi.
Kufuatia hoja za pande zote, Jaji Kaduri alisema atazitaarifu pande zote siku ya kutoa uamuzi wake baada ya kusikiliza maombi hayo pamoja na utetezi wa Jamhuri.
Hata hivyo, waandishi wa habari jana walipata wakati mgumu kutokana na kesi hiyo kuendeshwa katika chumba kidogo ambacho waliingia mawakili wa pande zote, Lwakatare, Jaji, mwandishi mmoja na viongozi wawili wa Chadema.
Watuhumiwa katika kesi hiyo ambao ni Lwakatare na Ludovick Rwezahula, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18, mwaka huu na kusomewa mashitaka manne yakiwamo ya ugaidi, katika kesi namba 37 ya mwaka 2013.
Aidha, wanatuhumiwa kula njama na kupanga kumteka Mhariri wa magazeti ya Mwananchi, Dennis Msacky na kisha kumdhuru kwa kutumia sumu. Hata hivyo, Machi 20, mwaka huu, DPP aliwafutia mashitaka washtakiwa hao lakini muda mfupi baada ya kutoka nje ya ukumbi wa mahakama, walikamatwa na kufunguliwa mashitaka hayo hayo katika kesi namba 6, ya mwaka 2013.
Uamuzi huo wa Mahakama kusikiliza maombi hayo katika 'chamber' badala ya mahakama ya wazi, ulizua manung’uniko na malalamiko kutoka kwa waandishi na wanachama wa Chadema na wafuasi wao, huku baadhi ya wafuasi wa Chadema wakiwaporomoshea matusi makali polisi waliokuwa wakilinda usalama mahakamani hapo.
Aidha, wakati Lwakatare akisikindikizwa na askari Magereza kurudishwa rumande, alinyoosha mikono na kuwaambia ndugu zake pamoja na wanachama wa Chadema kwamba Mungu yupo na siku moja ataibuka mshindi.
Alionekana mwenye furaha na muda wote alikuwa akitoa maneno ya kumuomba Mungu na kumuachia yote yaliyomkuta na kusema 'msiwe na wasiwasi Mungu yupo pamoja na nami.'
Akizungumza na umati mkubwa wa ndugu wa Lwakatare pamoja na wafuasi wa Chadema, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliyeongozana na Katibu wake, Dk. Willibrod Slaa, alisema anaamini haki itatendeka na anaiamini mahakama.
Hata hivyo, Mbowe alisema kesi hiyo imekuwa na msukumo mkubwa wa kisiasa na kwamba wataendelea kudai haki ili kuhakikisha inapatikana kupitia mahakama.
CHANZO: NIPASHE
Tuesday, April 16, 2013
MAWAKILI WA RWAKATALE WAISHUKIA MAHAKAMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment