KWA mara nyingine tena Mahakama ya Rufaa nchini, imetupilia
mbali maombi yaliyowasilishwa na walalamikaji, Musa Mkanga, Agnes Mollel
na Hapiness Kivuyo ya kutaka kupitia upya hukumu iliyomrejesha Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA).
Walalamikaji hao ambao ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
kupitia kwa mawakili wao, Alute Mughwai na Modest Akida, walidai
kutoridhishwa na hukumu hiyo iliyotolewa Desemba 21 mwaka jana.
Walikuwa wakidai kuwa kulikuwa na mapungufu katika hukumu hiyo, hivyo
walilitaka jopo la majaji waliohukumu kesi hiyo kukubali kubatilisha
uamuzi wao ili rufaa ya kesi namba 47/2012 waliyokuwa wamefungua
isikilizwe upya.
Wakili Mughwai aliitaka mahakama ifutilie mbali hukumu hiyo kwa madai
kuwa ilipingana kwa kiasi kikubwa na hukumu iliyotolewa katika Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha.
Akitoa mfano wa kesi zingine mbalimbali zilizowahi kupatikana na
mazingira kama kesi ya Lema, Mughwai alijikita katika kifungu cha 66(a)
na (b), na 4(ii), ambavyo majaji walimwambia amevichanganya vibaya
badala ya kufungua kila dai moja peke yake.
Hata hivyo wakili huyo alidaiwa kuwa kuna vifungu alikuwa anavisema kwa mdomo wakati hakuviweka katika maandishi.
Nao mawakili wa Lema, Method Kimomogolo, akisaidiwa na Tundu Lissu
walitoa utetezi kuwa maombi hayo yaliletwa kinyume cha utaratibu, hivyo
kutaka kuichanganya mahakama.
Walidai kuwa utaratibu uliotumika haukuwa sahihi, huku wakisisitiza
kuwa kosa ambalo upande wa waleta maombi haukuonyesha kosa wazi, kwani
kama lingekuwa dhahiri hakungehitajika kurasa 29 za maandishi kuelezea
kosa hilo.
Kimomogoro alisoma kwa uangalifu sababu 11 kujibu hoja za wakili
Mughwai na kwa umakini akilezea sababu za kutokuwepo kesi ya kujibu au
sababu za kupitia hukumu hiyo upya.
Kimomogolo adai, “Hatukuona kama ni suala la msingi kwa kuwa suala
lenyewe halikuwa wazi zaidi, hii ni kwa sababu msingi wa hoja ya kesi
(locus standi) ni wa muhimu katika kuanzisha kesi zozote za kisheria
katika mahakama.”
Kwamba kuna kesi ya kujibu au hakuna kisheria, alidai kuwa mahakama
ilikuwa sahihi iliposema kuwa suala la hoja ya msingi wa uwepo wa kesi
(locus standi) ni la umuhimu katika uendeshaji wa kesi kama hizo.
Aidha, pande zote mbili zilisema kuwa suala la walalamikaji kuwa
wapiga kura walioandikishwa kupiga kura katika uchaguzi ambao matokeo
yake yanalalamikiwa, vivuli vya vitambulisho vyao vya kupigia kura
vimewekewa alama A( l-J).
“Ni kweli kwamba wakili Mughwai aliwasilisha vitambulisho vya kupigia
kura kuthibitisha kuwa walalamikaji walikuwa ni wapiga kura
walioandikishwa, hayo yalijiri mahakamani Aprili 6, 2011,” alisema
Kimomogoro.
Aliongeza kuwa kwa bahati mbaya vitambulisho vya wapiga kura
havikutolewa na kukubaliwa na mahakama kama ushahidi kwa kanuni za
kimahakama na taratibu zake na hivyo katika kesi hiyo hakukuwepo na
ushahidi kwenye kumbukumbu za mahakama na majaji walipomwomba Mughwai
aionyeshe kama alifuata taratibu hizo hakuweza.
Hata hivyo pamoja na mivutano yote ya kisheria ya pande zote, jopo la
majaji watatu wakiongozwa na Jaji Engela Kilewo akisaidiwa na Bernard
Luanda na Salumu Masatti, waliyatulipia mbali maombi hayo ya kupitiwa
upya kwa hukumu hiyo kwa misingi kuwa haikuwa na nguvu kisheria.
Baada ya hukumu hiyo, wakili Mughwai alisema kuwa anaikubali hukumu ya
mahakama, huku Lissu akiwataka watu kuacha kutumika kufungua kesi.
Aliionya CCM iache kuwasumbua badala yake itumikie wananchi na isubiri uchaguzi mkuu 2015.
No comments:
Post a Comment