Tuesday, April 16, 2013

FILIKUNJOMBE AJA JUU ASEMA WATU WASIWE AKINA NAPE


MBUNGE wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), amesema kuwa serikali iliyoko madarakani si sikivu kuhusu matatizo ya wananchi.
Amesema kuwa baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakifanya mambo wanayotaka wao badala ya kujali masilahi ya wananchi wanaowaongoza.
Kwa sababu hiyo, Filikunjombe alikataa kuiunga mkono hotuba ya bajeti ya waziri mkuu, kwani baadhi ya mawaziri pamoja na kuapa kuitetea Katiba lakini wanaonekana kujilinda wao wenyewe na kuiweka Katiba pembeni.
“Mheshimiwa Spika, tuna mawaziri 60 hapa na kwa haraka haraka wanaofanya kazi ipasavyo hawazidi hata 10 na naweza kuwataja kwa majina. Siungi mkono hoja kwa sababu kila mmoja atakuwa shahidi kuwa serikali si sikivu, imekuwa na tabia ya kufunika kombe mwanaharamu apite,” alisema.

Mbunge huyo aliituhumu serikali kuwa imevaa miwani ya mbao na imeziba masikio yake, kauli iliyoonekana kumkera Spika, Anne Makinda, ambaye alimtaka afute kauli yake hiyo.
“Jamani hebu ondoa maneno hayo ya mbao, je, mbao inavaa miwani? Hebu ondoa maneno hayo tafadhali,” alisema Spika.
Mbunge huyo aliondoa maneno hayo akisema kuwa anamaanisha kuwa serikali si sikivu na kuendelea kuchangia hotuba hiyo.
Filikunjombe alisema elimu nchini imeshuka na kwamba takwimu zinaonesha kuwa ni kweli shule za sekondari zimeongezeka kutoka 1,700 hadi 4,000 na wanafunzi wanaofaulu wameongezeka kutoka laki nne hadi milioni 1.5.
Aliweka bayana kuhusu hilo kuwa halisaidii bali anaona kuwa ni afadhali kufaulisha wanafunzi hao laki nne kuliko milioni 1.5 wasiofahamu kusoma, kuandika na kuhesabu. 
“Tunafaulisha wanafunzi ambao hawajui kusoma na kuandika, ni bora kuwa na wachache wenye ubora badala ya kupeleka wengi wasiokuwa na ubora.
“Nashangaa kwanini tunapiga kelele mwaka huu kuwa wanafunzi wengi hawajafaulu badala ya kupiga kelele mwaka jana na mwaka juzi, ambapo walifaulu wasiojua kusoma na kuandika,” alionya.
Aidha alishangazwa na uanzishwaji wa utitiri wa tume za kuchunguza matokeo ya mitihani ambazo hata hivyo alidai hazina tija kwani mwaka 2010/2011 iliundwa kama hiyo na kutumia mamilioni ya fedha.
Alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa badala ya watu kuwajibika kwa kuhakikisha wanafanya kazi, zinaundwa tume nyingine kwa ajili tu ya kufunika kombe ili mwanaharamu apite.
Filikunjombe ambaye alionekana kuwaduwaza wabunge wenzake wa CCM, aliishukia serikali kwa kuweka michango mingi isiyo na tija huku ikidai kwamba imeondoa ada ya shule za msingi ya sh 3,000 lakini michango inafikia hadi sh 17,000.
Alisema kuwa ni bora wazazi wakatambua kuwa elimu si bure bali wajiandae kutafuta fedha kuliko kulipa michango mingi isiyo na idadi ambayo kiukweli inawaumiza kimaisha.
Aliongeza kuwa viongozi serikalini ambao wapo chini ya chama tawala hawapaswi kubeza mawazo ya kambi ya upinzani, badala yake wazichukue hoja zao, wazipime na kuzifanyia kazi.
Alisema kuwa wao wamepewa dhamana ya kuongoza na kuwatumikia wananchi wakiwamo wa vyama vya upinzani, hivyo hoja zao wazifanyie kazi, huku akishangazwa na namna wanavyotumia muda mwingi kuzibeza hoja hizo.
“Mheshimiwa Spika, sisi ambao ni chama tawala tufanye kazi, na kipimo chetu kiwe utendaji wetu…inashangaza tunaacha kuongoza tunafanya kazi za Nape Nauye, yeye atafanya kazi gani?
“Ndiyo maana kunatokea matusi bungeni kwani badala ya sisi kufanya kazi za wananchi tunafanya kazi za watu wengine,” alisema.
Mbunge huyo alitahadharisha viongozi wa serikali kuwa wapinzani na wananchi kwa ujumla wanawaelewa CCM, ambapo kama wangewatumikia inawezekana wangeacha kuwa wapinzani.
Kuhusu mahitaji ya wapiga kura wake, Filikunjombe alisema wanataka vitu vidogo tu, navyo ni meli ya uhakika zaidi ya MV Songea ambayo haifanyi kazi.
Matusi yamkera Spika
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge Anne Makinda, amewajia juu wabunge wanaoacha kujadili hoja na badala yake kuporomosha matusi.
Spika Makinda alisema hayo baada ya juzi baadhi ya wabunge waliokuwa wakijadili hotuba hiyo kuporomosheana matusi ya nguoni.
Akizungumza mara baada ya kipindi cha maswali na majibu jana asubuhi, Makinda alisema ameshangazwa na baadhi ya wabunge hao kuvaa suti, lakini matendo na kauli zao bungeni haziendani na hadhi ya suti zao.
Spika Makinda ambaye alionesha dhahiri kukerwa na hatua hiyo, alisema amepata ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kutoka kwa mwananchi mmoja, akieleza jinsi alivyokerwa na tabia ya wabunge ya kutoa matusi.
“Mwananchi mmoja amenitumia ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yangu ya mkononi akisema hivi: ‘Hili Bunge lenu sasa limezidi mpaka mnaitana… Hapa ametumia neno ambalo siwezi kulitaja maana sijui kutukana.
‘Kuanzia sasa sitathubutu kuangalia kipindi cha Bunge nikiwa na watoto. Itabidi nikae chumbani kuangalia na kusikiliza hayo matusi,”’ alinukuu ujumbe huo Spika.
Kwa mujibu wa Spika, kuanzia sasa mbunge yeyote atakayetoa lugha chafu bungeni atatumia mamlaka aliyonayo kuwaita polisi wamkamate.
Alisema hatua hiyo ataichukua kwa pande zote mbili, yaani wabunge wa chama tawala na wale wa upinzani.
“Jamani tumeanzisha vyama vingi si kuja hapa kutukanana. Jamani mmevaa suti vizuri lakini mnafanya mambo ambayo hayaendani na hadhi yenu,” alisema.
Juzi mjadala wa hotuba hiyo uliingia katika hatua mbaya baada ya baadhi ya wabunge wa CCM kuamua kumwaga matusi na kutoa lugha ya kejeli dhidi ya wenzao wa CHADEMA.
Aliyeanza kutoa lugha chafu na za kejeli ni Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), ambaye alisema kuna wabunge ndani ya Bunge hilo wamepata mimba bila kutarajia.

Pia Lusinde alimtusi Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kwamba ana mtoto wa wiki sita wakati yeye mtoto wake wa mwisho ana umri wa miaka minane.
Mbunge mwingine wa CCM, Juma Nkamia (Kondoa Kaskazini), naye alimtusi Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph Mbilinyi, kwa kumwita mbwa.
Wiki iliyopita Mbilinyi wakati akichangia mjadala wa hotuba hiyo alisema hajisikii fahari kuwa bungeni kufanya kazi pamoja na Mbunge aina ya Mwigulu Nchemba (CCM).
Alisema Mwingulu ni mpumbavu kwani amecheza dili ya ugaidi kuivuruga CHADEMA na kutuma fedha kwa njia ya simu.
Naye Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kingwangala (CCM), alitumia muda mwingi kushambulia na kutoa lugha chafu dhidi ya viongozi na wabunge wa CHADEMA.

No comments:

Post a Comment