Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi (kulia) akizungumza na wabunge wa Chadema baada ya kikao cha
kunge kualishwa jana mchana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Wabunge watano wa Chadema jana walitimuliwa bungeni na
kuamriwa kukaa nje ya Bunge kwa siku tano kutokana na vurugu zilizotokea
jana usiku.Wabunge hao ni Lissu, Hezekiah Wenje (Nyamagana), Highness
Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) Godbless Lema (Arusha
Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).
Chanzo za kufukuzwa kwao ni kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje Lissu ambaye alikuwa ameamriwa kutoka nje na Naibu Spika, Job Ndugai baada ya kuingilia hotuba ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba.
Kutokana na tafrani hiyo, Nchemba hakuweza kuhitimisha hotuba yake hivyo Ndugai alilazimika kukatisha mkutano wa Bunge.Hata hivyo wakati akiahirisha mkutano huo, tayari wabunge hao walikuwa wameshatolewa nje baada ya askari kuongezwa.
Mapema Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alitoa tusi zito la nguoni wakati wa hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, licha ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kupiga mkwara wa kuwashughulikia wabunge watakaorusha matusi.
Mbali na tukio hilo Lema naye alichafua hali ya hewa baada ya kuwatuhumu viongozi wa CCM akiwamo Rais Jakaya Kikwete kwa udini, madai ambayo Bunge limempa siku saba kuyathibitisha.
Lema aliituhumu CCM na Serikali yake chini ya Rais Kikwete kwa kushindwa kutatua mgogoro wa kidini na badala yake kuwa kama analikwepa tatizo. Alionya kuwa Taifa linapasuka kwa migogoro kutokana na viongozi wa Serikali kushindwa kulishughulikia.
Kauli iliwanyanyua vitini Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu na Sera), William Lukuvi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Lukuvi na Jaji Werema walisimama wakidai kuwa Lema alikuwa amemdhihaki Rais Kikwete kwa kauli zake za kumhusisha na masuala ya udini.
Hata hivyo, Mnadhimu Mkuu wa Upinzani, Lissu alisimama kumtetea Lema akidai hakuwa amemdhihaki Rais bali alikuwa amemkosoa kitu ambacho kanuni za Bunge zinaruhusu.
Lema aliruhusiwa kuendelea na hoja yake na ndipo akamtolea mfano Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira wakati alipokwenda Mwanza kutatua mgogoro baina ya Wakristo na Waislamu kuhusu suala la kuchinja.
“Wassira akifahamu yeye ndiye, Waziri alikwenda Mwanza na kuwaacha viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu watatue wenyewe suala la kuchinja. Sasa alitaka diwani atatue mgogoro ule?”
Baada ya kumaliza kuchangia, Naibu Spika alitangaza kuwa Lema anatakiwa kuwasilisha katika muda wa siku saba uthibitisho kuwa Rais anahusika na tatizo la udini.
Serukamba
Serukamba alipewa nafasi ya kutoa taarifa wakati wabunge walipokuwa wakilumbana juu ya uhalali wa Msemaji wa Upinzani, Profesa Kulikoyela Kahigi kuzungumzia bungeni masuala yaliyoko mahakamani na shughuli za Idara ya Usalama wa Taifa.
Wakati akijiandaa kusoma vifungu vya kukatiza hotuba ya Profesa Kahigi, alitukana tusi zito la nguoni kwa lugha ya kimombo ambalo kwa sababu za kimaadili hatukuweza kuliandika, kisha akaendelea kuzungumza huku baadhi ya wabunge wakipigwa butwaa.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai aliyekuwa akiongoza shughuli za Bunge wakati huo, hakutoa karipio lolote huku akimruhusu Serukamba kuendelea kwa muda kabla ya kumkatiza na kumruhusu Mbunge wa Simanjiaro (CCM), Christopher Ole Sendeka kuzungumza.
Ubishi ulivyoanza
Muda mfupi kabla ya Profesa Kahigi kuanza kusoma hotuba yake, Serukamba alisimama na kuomba mwongozo wa Spika kupitia Kanuni ya 68(1) akitaka isisomwe kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa nne kwa kuwa unaingilia uhuru wa Mahakama... “Ni juzi tu Akoonay (Mustapha, Mbunge wa Mbulu - Chadema), alitukumbusha kwamba mambo hayo ni ‘prejudice’ kwa Mahakama kwa hiyo ukiruhusu hilo Naibu Spika itakuwa ni ajabu.”
Kabla Naibu Spika hajatoa mwongozo wake, alimtaka Profesa Kahigi kuzungumza kama anakubaliana na Serukamba, lakini Profesa Kahigi alisema anaomba kuendelea kusoma hotuba yake kama ilivyo.
No comments:
Post a Comment