Tuesday, April 23, 2013

AMCHINJA MAMA YAKE KWA TUHUMA ZA UCHAWI

MKAZI wa Kijiji cha Chombwe wilayani Ileje, Michael Panja amemuua mama yake mzazi, Anna Panja (60) kwa kumchinja shingo na kisu akimtuhumu uchawi.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakeli Masaki, tukio hilo lilitokea Aprili 23 mwaka huu, saa saba usiku katika Kijiji cha Chombwe.

Masaki aliwaambia waandishi wa habari kuwa mama huyo alikutwa ameuawa kwa kuchinjwa shingoni kwa kutumia kisu na watu wawili akiwemo mtoto wake huyo.

Alisema kuwa Michael akiwa na mwezake ambao hawakuweza kufahamika mara moja, walikwenda nyumbani kwa mama huyo na kumvamia akiwa amelala na mumewe, Basale Panja (76) na kumkamata kisha kumchinja shingo.

Masaki alisema chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina ambapo mtoto huyo alikuwa akimtuhumu mama yake mzazi kuwa ni mchawi na kwamba amekuwa akimroga mkewe.
Aidha, alisema watuhumiwa wote wawili wanatafutwa na polisi baada ya kufanya tukio na kukimbia.

Katika tukio la pili, mkazi wa Kijiji cha Kandete wilayani Rungwe, Lufingano Nsinge (32) aliuawa kwa kupigwa na kundi la wananchi kwa tuhuma za kuhusishwa na mauaji ya watoto wadogo yanayoendelea katika eneo hilo.
Alisema kuwa Nsinge alikutwa ameingia nyumbani kwa John Mwasammaleba kwa lengo la kutenda kosa hilo lililohusishwa na mauaji ya watoto.

Hata hivyo, katika tukio hilo watu wanne wanashikiliwa na polisi na kwamba uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.


No comments:

Post a Comment