Ndugu zangu habari za
wikiendi. Yapo mambo machache ningependa kuwashirikisha ili kuweka
kumbukumbu sawa na pia kuzuia upotoshaji ambao unaweza kujitokeza siku
za usoni iwe kwangu, kwako au kwa mtu mwingine.
Mojawapo ya mambo makubwa
ambayo yamejitokeza siku za karibuni hasa katika suala la Teknolojia na
habari ni jambo la sheria za faragha (privacy and privacy lawas).
Tumeshuhudia kufungwa kwa gazeti za News of The World, mali ya bilionea
Rupert Murdoch wa Kimarekani baada ya kudhihirika alitumia wataalam wa
teknolojia (hackers) kutafuta siri za watu mashuhuri kwa kuingia katika
simu zao za mkononi kinyume cha utaratibu na sheria za faragha (Privacy
Laws). Tumeshuhudia pia wahalifu hao hao wa mtandao wakifanya mengi kama
kuvamia kwa mitandao ya makampuni makubwa kama Sony na mengineyo na
hata katika mitandao hii ya kijamii upo wakati marafiki zako wanakwambia
mbona umenitumia kitu kisichoeleweka, na baadaye kuja kugundua kwamba
si wewe uliyefanya hivyo.
Tarehe 1, 8 na 9 mwezi huu
wa Machi nilikuwa Dar es Salaam kwa shughuli zangu za kawaida kimaisha
lakini ziko updates 5 zilifanyika hapa moja ikimhusu ndugu Absalom
Kibanda. Ni ajabu kwamba baadhi ya waandishi tena waliojivika taji la
usahihi katika uandishi waliiandika habari hiyo bila hata kuniuliza
kwamba ni nini kinatokea. Tunajitahitahidi na kutamani kuwa na Taifa la
waandishi makini na wenye kufuata maadili lakini wapo wanaoturudisha
nyuma. Ni ajabu gazeti kuandika jambo lisilo la kweli huku wahusika
wakiwa na kila uwezo wa kumfikia yule wanayedhani kwamba ameandika na
kumhoji ili kuhakiki habari. Kazi ya uhariri ni kuhakiki. Ikiwa mtu
atakimbilia kuandika jambo likuhusulo ambalo hana hakika nalo na alikuwa
na kila uwezo wa kuwasiliana na wewe na kukuuliza lazima utajiuliza
maswali mengi. Kwanza: Nini hasa lengo lake na pili ufahamu wake wa kile
anachokifanya kwa maana ya taaluma yake katika kazi anayoifanya.
Napenda kuwaambia kwamba
katika tarehe tarehe hizo mwezi huu wa Machi, wahalifu wa mtandao wakiwa
eneo la Njiro na baadaye Kijenge mjini Arusha (Kila post ilionyesha
eneo ilipotoka), (wakati huo mimi nikiwa Dar es Salaam) waliingia bila
idhini kwa njia haramu (Hacking) katika anuani yangu ya Facebook na
ku-post habari hizo tano. Sasa nimeliacha jambo hilo katika vyombo
stahiki vya ulinzi na usalama ili kufuatiliwa kadiri ya taratibu zao.
Natoa wito kwa ndugu zangu
waandishi kujitahidi kuhakiki habari kabla ya kuzipeleka katika vyombo
vyao. Hii itasaidia 1. Wao kujenga heshima mbele ya jamii 2. Kufikisha
kile hasa ambacho ni habari 3. Kuzuia mikanganganyiko isiyo ya lazima.
Haya yakizingatiwa nadhani hata sintofahamu hizi za uandishi wa habari
unaotokana na hisia na vyanzo vumbi na ufahamu mdogo wa jambo
utaondoka na tutakuwa na jamii ambayo haki na uwajibikikaji wa
wanahabari kwa jamii utaonekana kutendeka
Niombe radhi kwa ndugu
yangu, rafiki yangu na pia mwalimu wangu, Ndugu Absalom Kibanda kwa
usumbufu wowote uliojitokeza ambao naamini watu wasio na nia njema
walitaka kuutumia kuleta hisia tofauti katika jamii na pia kumpa pole
kwa mara nyingine tena kwa maumivu yaliyosababishwa na ujangili huo.
Namuombea kwa Mungu ampe unafuu mapema zaidi ili arudi katika meza yake
kuendeleze harakati za kupambana na mchango wake katika kuleta maendeleo
ya kweli kwa nchi yetu. Pili, pole pia kwa wote ambao kwa namna moja au
nyengine walikwazwa na uzushi huo, kwa kuwa sina tatizo lolote na Bwana
Kibanda na wala nisingependa lililomtokea limtokee yeye wala mtu
mwengine yeyote.
Ni imani yangu ya dhati
kwamba vyombo husika katika nchi yetu havitasita kulitalifanyia kazi
jambo hili na ukweli juu ya nini kimemtokea Bwana Absalom Kibanda
utajulikana na kuwekwa bayana.
Mwisho, shukrani kwa wote
mlionipigia simu kuhusu hili, tuko pamoja na nawatakia kila la kheri
katika shughuli za ujenzi wa Taifa letu hili la Tanzania ambalo msingi
wake umejengwa katika haki, umoja, amani na kujali hali za watu wake.
No comments:
Post a Comment