Saturday, February 2, 2013

UJUMBE WA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA ARDHIOEVU DUNIANI TAREHE - 2 FEBRUARI 2013


 Ardhioevu Hutunza Maji
 MIKOKO NI SEHEMU YA ARDHIOEVU
Mhe. Khamis S. Kagasheki Waziri wa Maliasili na Utalii
Ndugu Wananchi,
Tarehe 2 Februari kila mwaka ni siku ya Ardhioevu Duniani (World Wetlands Day).
Katika siku hii watu duniani kote wanatafakari na kukumbushana umuhimu wa Ardhioevu katika maisha yao ya kila siku.
Kauli mbiu ya siku ya Ardhioevu Duniani mwaka huu ni ‘Ardhioevu hutunza maji’. Hii ni kutukumbusha nafasi ya ardhioevu katika kuhakikisha kuwa maji yanakuwepo siku zote na kwa vizazi vyote.
Siku ya ardhioevu Duniani inaadhimishwa Kitaifa mjini Babati Mkoani Manyara ambako Mkuu wa Mkoa atakuwa mgeni rasmi. Maandalizi ya maadhimisho hayo yameratibiwa na Klabu za Malihai kutoka shule za Msingi, Sekondari na vyuo mbalimbali.
Shughuli mbalimbali zitafanyika mjini Babati katika kuadhimisha siku hii muhimu,  kama vile;
(i) Kupanda miti;
(ii) Kuhudhuria semina ya ardhioevu;
(iii) Kuhamasisha wananchi kwa njia ya maonyesho ya sinema;
(iv) Kuzindua kitabu cha uenezi kuhusu mazingira.
Kaulimbiu ya Kimataifa isemayo ‘Ardioevu hutunza maji’ imekuja wakati muafaka ambapo Taifa letu linatekeleza Programu ya ‘KILIMO KWANZA’ ambacho, pamoja na mambo mengine, hufanikishwa na ardhioevu, hususan kilimo cha umwagiliaji. Wote tunajua kuwa kilimo cha umwagiliaji ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa chakula kinapatikana kwa watu wote mwaka mzima (food security).
Hivyo, nachukua fursa hii kuwahimiza wananchi kutunza vyanzo vya maji. Yaani, watu wasifanye shughuli zozote katika sehemu hizo, kama vile kulima na kuchungia mifugo katika misitu inayohifadhi maji.
Kwa kutambua umuhimu wa ardhioevu, mwaka 2000 Tanzania iliridhia Makubaliano ya Ramsar (Ramsar Convention) yenye nia ya kuhifadhi na kuendeleza sehemu za ardhioevu. Maeneo makuu manne ya Ramsar yaliyotengwa  hapa nchini ni kama yafuatavyo:
(i) Malagarasi Moyowosi;
(ii) Ziwa Natron;
(iii) Bonde la Kilombero;
(iv) Eneo la Rufiji-Mafia-Kilwa.
Maeneo hayo ni kati ya yale yanayohifadhiwa hapa nchini kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.
Nachukua fursa hii kuwashukuru watu wa Kilombero na Ulanga kwa kukubali kuondoka na mifugo yao kutoka katika Bonde la Kilombero.
Pamoja na kuhifadhi maji, Bonde la Kilombero lenye ukubwa wa Hekta 7,950, ni maarufu kwa kuhifadhi mnyama Puku ambaye yuko kwenye hatari ya kutoweka duniani. Hata hivyo, kwa kuwa sasa Bonde la Kilombero halitakuwa tena na mifugo itakuwa fursa nzuri ya kuzaana kwa Puku.
Ningependa kusisitiza pia kuwa utunzaji wa ardhioevu sharti uambatane na utunzaji wa misitu maana miti na mimea husaidia maji kunywea ardhini na baadaye kutokeza juu ya ardhi kama vyanzo vya maji. Maji hayo ndiyo huingia kwenye ardhi chepechepe, visima, mito na mabwawa.
Mwisho ningependa kuchukua fursa hii kusisitiza umuhimu wa ardhioevu:
(i)     Ardhioevu ni chanzo cha maji tunayotumia nyumbani na viwandani;
(ii)  Asilimia 60 ya umeme hapa nchini hutokana na maji yanayoanzia kwenye ardhioevu;
(iii)                       Kilimo cha umwagiliaji, kama vile mpunga na mboga, hufanikishwa na ardhioevu;
(iv)                       Wanyamapori hutegemea ardhioevu kupata maji;
(v) Ardhioevu hufanikisha uvuvi katika mito na mabwawa.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu hapa nchini hutegemea ardhioevu katika maisha yao ya kila siku.
Kwa upande mwingine inakadiriwa kuwa karibu asilimia 50 ya ardhioevu imevamiwa na watu kwa ajili ya kilimo na kuchungia mifugo.
Natoa wito kuwa watu wote ambao wanaishi, kulima na kufugia mifugo katika maeneo ya ardhioevu ambayo yamehifadhiwa wanatakiwa kuhama kama wanavyoshauriwa na Serikali.
Wizara ya Maliasili na utalii itaendelea kushirikiana na wananchi, wafadhili na wadau mbalimbali katika juhudi za kuhifadhi na kutunza ardhioevu.
Namalizia kwa kusema ‘Ardhioevu hutunza maji’ tutumie ardhioevu kiundelevu.

Mhe. Khamis Kagaseki
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII.
2 Februari 2013

No comments:

Post a Comment