Monday, February 18, 2013

MAMA ALIYEMTESA MTOTO MBEYA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA JELA

Mtoto Aneth mara baada ya kukatwa mkono wa kushoto kwa ujumla mtoto huyu anaendelea vizuri na alishatoka hospitalini

Wilvina Mkandala (24) akitolewa mahakamani mara tu baada ya kusomewa hukumu ya kifungo cha maisha 

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mbeya imemhukumu kifungo cha maisha Wilvina Mkandara(24) kutokana na kesi iliyokuwa inamkabili ya kumtesa hadi kumsababishia ulemavu mtoto wa shemeji yake.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu mkazi wa mahakama hiyo Gilbert Ndeuruo alisema mshakiwa amehukumiwa kutokana na kifungu cha 235 cha mwenendo wa makosa ya jinai cha mwaka 1985.

Amesema Mahakama inaweza kumtia hatiani mtuhumiwa kutokana na ushahidi wa mazingira au ushahidi wa moja kwa moja ambapo alisema mshtakiwa anahukumiwa kutokana na ushahidi wa mazingira kwa sababu mhangwa wa tukio hilo alishindwa kutoa ushahidi wa moja kwa moja.
 
 
Ameongeza kuwa mahakama hiyo imeona mshtakiwa anastahili adhabu kutokana na mtuhumiwa huyo kama mzazi kushindwa kujali afya ya mtoto ili hali alikuwa mama mlezi ikiwa ni pamoja na kumpeleka Hospitali kwa wakati ili apatiwe matibabu.
Ndeuruo amesema pia mahakama hiyo haikuridhishwa na na ushahidi wa mtuhumiwa alioutoa mahakamani kuwa majeraha yaliyokutwa mwilini mwa mhanga wa tukio hilo yalitokana na kuugua kwa tetekuwanga jambo ambalo alisema si la kweli.

Amesema kuwa mshtakiwa ametoa maelezo wakati wa utetezi wake yanayopingana na na maelezoya daktari aliyemtibu mgonjwa alipofikishwa hospitali wakati akitoa ushahidi mahakamani hapo.

Hata hivyo kabla ya kutoa hukumu hiyo Hakimu huyo alisema kutokana na ibara ya 16 ya sheria ya African Charter inayotaka Nchi itunge sheria ya kulinda haki za watoto ambapo Tanzania haina sheria hiyo hivyo kusababisha watu kuwanyanyasa watoto.

 
Hakimu huyo ametoa wito kwa taasisi zinazohusika kutunga sheria hiyo mara moja ili kulinda haki za watoto ambayo itatamka wazi adhabu kwa wale watakaobainika kuwatesa na kuwanyanyasa watoto.
Kwa upande wake mwendesha mashtaka wa Serikali Archiles Mulisa ameiiambia mahakama hiyo kumpa adhabu kali mtuhumiwa huyo ili liwe fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia kama hizo ambao hajakamatwa.

Amesema kitendo kilichofanya na mshtakiwa huyo ni kitendo chakinyama ambacho kinatakiwa kulaaniwa vikali hivyo kupitia adhabu atakayopewa mtuhumiwa inaweza kupunguza unyasasaji kama huyo katika jamii.

Aidha mshtakiwa Wilvina alipotakiwa kujitetea ili apunguziwe adhabu kabla ya kusomewa aliomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kile alichodai kuwa ni mjamzito, pia hajui mtoto wake aliyemzaa alipo pamoja na mawasiliano na familia yake.
 
Akitoa hukumu hiyo hakimu Ndauruo amesema amesikitishwa na kitendo cha mtuhumiwa cha kuomba kupunguziwa adhabu kutokana nakutomwona mtoto wake hali inayoonesha kutomjali mtoto aliyemtendea kosa.

Ameongeza kuwa Mahakama imefuatilia historia ya nyuma ya mtuhumiwa ambayo haioneshi kama anamatukio kama hayo ambayo aliwahi kuyafanya lakini mtuhumiwa anastahili adhabu kali kama upande wa mashtaka ulivyo sahauri na kutokana na mhanga kuwa na ulemavu wa kudumu.

Amesema mahakama inamhukumu kifungo cha maisha kifungo kitakachothibitishwa na mahakama kuu kutokana na mtuhumiwa kuwa na haki ya kukata rufaa kama ameona ameonewa katika kesi hiyo.

Mwanamke huyo alipandishwa kizimbani Novemba 16, Mwaka chini ya Mwendesha mashtaka wa Serikali, Achiles Mulisa aliiambia Mahakama kuwa Mtuhumiwa Wilvina Mkandala (24) alitenda kosa la kusababisha majeraha akiwa na nia ovu ambayo imemsababishia ulemavu mtoto Aneth.
NA MBEYA YETU BLOG


No comments:

Post a Comment