Monday, February 4, 2013

HOA YA MNYIKA HII HAPA


Mbunge wa (Ubungo) John Myika akiwasilisha hoja binafsi juu ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika jiji la Dar es salaam Bungeni leo.Picha na Mwanakombo Jumaa -MAELEZO
---
Mheshimiwa Spika; 
Awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wa kuwawakilisha wananchi, kuisimamia serikali, kuidhinisha mipango na kutunga sheria.

Mheshimiwa Spika;
Aidha, kwa namna ya pekee ni kushukuru wewe binafsi na uongozi mzima wa Bunge kwa kunipa fursa hii adimu na adhimu ya kuwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni ya 54 fasili ya (1) ya kupendekeza bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

Mheshimiwa Spika;
Maji ni uhai, hivyo matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam na nchini kwa ujumla kama hatua za haraka zisipochukuliwa yatageuka kuwa janga la taifa. Katika kila watanzania katika Jiji la Dar es Salaam na nchini; kwa wastani mmoja hapati huduma ya maji safi na salama na hali ni mbaya zaidi kuhusu ushughulikiaji wa maji taka.

Wakati baadhi ya nchi duniani zikielezwa kwenye kitabu cha hivi karibuni cha Mnukuzi Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN Special Rapporteur) kuwa katika mwelekeo unaostahili kuhusu kuhakikisha haki ya maji na usafi wa mazingira (On the right track; Good practices in realizing the rights to water and sanitation: 2012), hali ni kinyume kwa taifa letu.

Ripoti ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya maji (WaterAid: 2011) imeiweka Tanzania katika kundi la nchi ambazo haziko katika mwelekeo unaostahili wa kuboresha upatikanaji wa maji safi, ushughulikiaji wa maji taka na usafi wa mazingira (Policy Report: Off Track, Off Target; why investments in water, sanitation and hygiene is not reaching those who need the most).

Mheshimiwa Spika;
Hoja hii inalengo la kuibua mjadala wa hatua za haraka. Kimsingi hatua hizi za haraka hazitanufaisha Mkoa mmoja pekee kwa kuzingatia kuwa Mpango Maalum wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam ni kwa ajili pia ya maeneo mengine ya miradi iliyo sehemu ya mpango huo ya Morogoro mpaka Pwani. Aidha, kujadiliwa na kupitishwa kwa mapendekezo ya hoja hii kutaongeza pia msukumo wa miradi katika maeneo mengine ya mijini na vijijini katika mikoa mbalimbali nchini.

Shukrani zangu za dhati ziwafikie wabunge wenzangu wa vyama vya upinzani na wa chama tawala kwa maoni na mapendekezo yenu yaliyoniwezesha kuirekebisha hoja hii pamoja na ushauri wa Katibu wa Bunge Dr Thomas Kashillilah na maafisa na watendaji katika ofisi ya bunge, kambi rasmi ya upinzani na ofisi ya mbunge wa Jimbo la Ubungo mlioboresha hoja hii kwa manufaa ya Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika;
Nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi mnaoendelea kuniunga mkono kwa hali na mali katika kutimiza majukumu yangu ya kibunge na nafasi nyingine ninazozitumikia.

Nawashukuru sala zenu wakati wa kesi ya msingi na rufaa ya kupingwa kwa matokeo ya ushindi wetu Jimbo la Uchaguzi la Ubungo; kwa pamoja tumeshinda, tuendelee na kazi.

Aidha, pamoja na mjadala huu wa bungeni natarajia kupokea maoni na mapendekezo yenu kuhusu hoja hii kwa njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo kupitia mtandao wa www.mnyika.blogspot.com kwa hatua zaidi. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.Kusoma Zaidi Bofya na Endelea......>>>>>

No comments:

Post a Comment