Thursday, February 14, 2013

AJIRA ZA WALIMU ZA ZATANGAZWA



Serikali imetangazwa kuwa  imeajiri walimu wapya 26,537 kwa mwaka 2012/2013 watakaosambazwa katika shule mbalimbali kukabiliana na uhaba wa walimu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alitangaza ajira hizo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema kuwa walimu hao watasambazwa katika shule za sekondari, msingi na vyuo vya ualimu.
Dk. Kawambwa alisema waliopangiwa shule za msingi ni 13,527, walimu 12,973 wamepangiwa sekondari  na vyuo vya ualimu na 41 wamepangiwa shule za msingi za mazoezi zilizopo chini ya wizara.
Alisema katika ajira hizo, walimu wa cheti ni 13,568, shahada ni 8,887 na stashahada ni 4,086 na kuwa mwaka huu idadi imeongezeka kwa asilimia 11 sawa na ongezeko la walimu 2,630 ukilinganisha na mwaka 2011/12 ambao walimu walioajiriwa ni 23,907.
Alisema ajira hizo zimejumuisha walimu 841 wa stashahada waliofeli mwaka 2011 na kurudia mitihani yao na walimu 200 wa shule za msingi waliokuwa katika soko na kuomba ajira serikalini.
Dk. Kawambwa alisema walimu hao wanatakiwa kuripoti ofisi za wakurugenzi wa halmashauri walizopangiwa na kwa wakuu wa vyuo Machi Mosi mwaka huu.
Alisema mwisho wa kuripoti ni Machi 9, mwaka huu watakaoshindwa kuripoti nafasi zao zitapangiwa walimu wengine.
 Naibu Waziri wa wizara hiyo,  Philipo Mulugo, alisema walimu wote walioajiriwa watalipwa posho zao kama kawaida kulingana na utaratibu uliowekwa na serikali.
Mulugo aliwakumbusha walimu hao kuwa serikali itaendelea kuwachukulia hatua watakaokiuka taratibu za ajira ikiwamo ubadhirifu alitolea mfano kuwa mwaka jana aliwasweka rumande walimu 11 kwa makosa mbalimbali.

No comments:

Post a Comment