Saturday, December 22, 2012

STARS VS CHIPOLOPOLO LEO




MABINGWA wa soka barani Afrika, timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ leo wanashuka kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kuumana na wenyeji wao, Taifa Stars, katika mechi kali ya kirafiki ya kimataifa huku kila moja ikitaka kushinda. Chipolopolo waliobeba ubingwa wa Afrika Februari mwaka huu kwa kuwafunga Ivory Coast, jijini Libreville, Gabon, wamekamia kushinda kulinda heshima yao.
Mbali ya ubingwa wa Afrika, Zambia inashuka dimbani siku mbili tu tangu Shirikisho la Soka Afrika (Caf), litangaze kuwa ndio timu bora ya 2012.
Wakati Kocha wa Zambia, Mfaransa Herve Renard akiwataka vijana wake kushinda mechi ya leo kulinda heshima yao, Kim Poulsen wa Stars wa Stars, amesema watajitahidi kushinda mechi hiyo.
Kwa upande wa ubora wakati Zambia ikiwa nafasi ya 34, kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Tanzania ni ya 130.
Kwa upande mwingine makocha na manahodha wa timu hizo, wameahidi soka ya kiwango cha juu hivyo wakiwataka wapenzi na mashabiki kufika kujionea.
Poulsen alisema ni imani yake kwamba kikosi chake kitafanya kweli katika mechi ya leo, ingawa anatambua ubora wa Chipolopolo.
“Tumejipanga vya kutosha na kama mjuavyo, siku nyingi tuko kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huu na pia najivunia chipukizi kama Frank Domayo, Simon Msuva na wengine, naamini watafanya vizuri,” alisema Poulsen.
Kwa upande wa kipa na Nahodha wa Stars, Juma Kaseja, amewataka wapenzi na mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti.
Naye Kocha Msaidizi wa Zambia, Patrick Beaunelle, alisema watashuka dimbani kucheza kwa juhudi kubwa sio tu kushinda, bali pia kupata picha ya maandalizi yao kuelekea kampeni za kutetea ubingwa wao wa fainali za Afrika.
Kauli hiyo ni kama ile ya nahodha wa timu hiyo, Chris Katongo, aliyesema Stars ni kipimo kizuri kwao kabla ya kwenda Afrika Kusini kwa fainali za Afrika.

No comments:

Post a Comment