Friday, November 2, 2012

WAHADZABE: Wawindaji wa mwisho waliobaki Afrika



Wahadza au Wahadzabe kama wanavyofahamika, ni moja ya makabila madogo zaidi linalopatikana kaskazini mwa Tanzania kando ya ziwa Eyasi kwenye bonde la ufa na kupakana na uwanda wa Serengeti. Idadi ya Wahadza ni chini ya watu 1000 ambapo kati ya Wahadza 300-400 ni wawindaji na wakusanyaji mpaka sasa kama mababu zao walivyoishi kwa miaka zaidi ya 10,000. Wahadza wanabaki kuwa jamii ya mwisho kabisa barani Afrika inayotegemea uwindaji na ukusanyaji kwa ajili ya kuishi.


Kwa kuhtasari tu, haya ni baadhi ya mambo kuhusu Wahadzabe ambayo pengine huyafahamu;
  • Hawana uhusiano wowote wa kijenetiki na jamii yoyote ile japo wanawekwa kwenye kundi la ligha za Kikhoisan (Kusini mwa Afrika) kwa sababu ya lugha yao kuwa na sauti ya ``klik`` japo ni tofauti na katika nyanja zote.
  • Moja ya makabila yenye idadi ndogo zaidi ya watu, ikiwa na idadi ya wtu isiyofikia 1000 ambapo kati ya Wahadza 300-400 wanategemea uwindaji na ukusanyaji kama babu zao. 
  • Jamii pekee iliyobaki Afrika ambayo bado inategemea uwindaji na ukusanyaji, kama babu zao maelfu ya miaka iliyopika
  • Pamoja na Wasandawe walio umbali wa KM 150 kusini mwa ziwa Eyasi, Wahadza ni jamii pekee ambayo asili yao ni Tanzania. Ikumbukwe kuwa jamii zingine (Wabantu, Wakushi na Wanailoti) wameingia Tanzania wakitokea pande zote za Afrika
  • idadi yao ilipungua zaidi katika karne ya 19 baada ya ardhi yao kuvamiwa na jamii za wafugaji na wakulima
  • Jitihada za serikali ya kikoloni, baadaye serikali ya Tanzania na wamishionari za kuwajengea makazi maalum na yakudumu, kuwafanya wawe wakulima na kuwabadili kuwa Wakristo kwa sehemu kubwa zilishindikana. Mpaka sasa wahdza wengi huishi kama babu zao maelfu ya miaka. 
  • Wapo katika hatari ya kupoteza asili yao au kutoweka kabisa hasa baada ya ardhi yao kuvamiwa na wakulima na wafugaji, utalii na uwindaji wa kitalii unaofanywa katika maeneo yao ya asili
  • Japo kumeripotiwa wanawake wa Kihadza kuolewa na jamii za kibantu(wanyisanzu) na wadatoga lakini mara zote ndoa hizo huvunjika na wanawake wa kihadzabe kurudi kwa wahadza. Wanaume wa kihadza hawana tabia ya kuoa nje ya wahadza
  • Hujenga nyumba za muda zinazohamishika kirahisi (mobile houses), na nyumba hizi hujengwa na wanawake na wanawake ndio wenye maamuzi ya kuhama hasa pale wanapofanikiwa kupata mawindo ya mnyama mkubwa.
  • Wanaume ndio wawindaji na huoa mke moja tu. Tofauti na jamii za Kiafrika hapo zamani, Wahadza hujichagulia wenza wao wenyewe kwa kuangalia vigezo ambavyo ni uchapa kazi na mvuto au mwonekano.
  • Wahadza humiliki mali katika mfumo wa kijima. Wanapopata mawindo, wahadza hutoa zaidi ya 75% ya mawindo kwa jumuiya na familia husika hubaki na 25% (kiwango kikubwa zaidi katika mfumo wowote wa kodi unaofahamika duniani)
  • Mwaka 2007 serikali ilimilikisha eneo lenye kilometa za mraba zaidi ya 6,500 kwa familia ya kifalme ya Al Nahyan ya Muungano wa Falme za Kiarabu (United Arab Emirates) kwa ajili ya mapumziko yake na utalii  katika ardhi ya wahdza, hatua iliyopelekea Wahadza na Wadatoga waliokuwa wakiishi maeneo hayo kuondolewa kwa nguvu. Wahdza walipinga na wengine walifungwa. Hatimaye baada ya vyombo vya habari vya kimataifa kurepoti kuhusu hali hiyo, mpango hou ukasitishwa.
  • Eneo la Mang`ola lililopo kwenye bonde la Yaeda limegezwa kuwa wazalishaji wakuu wa vitunguu katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, sensa ya mwaka 1988 ilionesha kulikuwa na watu chini ya 2000 huko Mang`ola, baada ya kuanza kilimo cha vitunguu idadi ya watu iliongezeka na kufikia 38,000 mwaka 2002 na inakadiriwa kuwa sasa kuna zaidi ya wati 50,000 na hivyo kuathiri maisha ya Wahadza
Wageni wakitembelea nyumba ya Wahadza kwenye kituo cha 4CCP


Yapo mengi sana kuhusu Wahadzabe, ambao wanapatikana katika bonde la yaenda katika wilaya za mbulu, Iramba na Karatu. Jitihada za dhati zinafanya na Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni cha Haydom (4CCP) katika kuhifadhi na kulinda urithi huu ili usitowke. Kwa pamoja wamekusanya vitendea kazi vyao na wameandika historia yao na kujenga nyumba zao za asili katika kituo hicho kilichopo Haydom

No comments:

Post a Comment