Wednesday, November 21, 2012

SIMIYU: WATAKA RAIS AKABIDHI MADARAKA KWA JAJI

  Baadhi yaWananchi wa Kata ya Lamadi,  mkoani Simiyu wakitoa maoni

BAADHI ya Wananchi wa Kata ya Lamadi,  mkoani Simiyu wamesema ili kuwa na uchaguzi huru na haki, wakati wa Uchaguzi Mkuu Rais akabidhi madaraka kwa Jaji Mkuu ama Mwanasheria Mkuu.

Walisema kitendo cha kuingia kwenye uchaguzi mkuu , huku Rais aliyeshika madarakani akiwa bado hajayaacha, kunakuwa na ushawishi ama upendeleo.“Wakati Rais akiwa anavunja Bunge ili nchi iingie kwenye uchaguzi, yeye pia akabidhi nchi kwa Jaji Mkuu  kwa sababu hata Rais akichaguliwa ataapishwa na Jaji Mkuu,” alisema Alfred Mtumba (49).

Alisema Rais akiingia kwenye uchaguzi akiwa na madaraka yake hawezi kuwatendea haki wenzake anaoshindana nao.

Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Christina alisema anawanyima watu haki kwa kushika wadhifa wa mwenyekiti wa chama chake.

Alisema kwa Rais kuwa mwenyekiti wa chama, kunawanyima haki wananchi wa kawaida kutoa maoni yao.

Alisema pia kuwa wabunge wa kuteuliwa wakati wakiwa bungeni wawe wasikilizaji tu na siyo kuwa wachangiaji.
Pia alisema  wabunge hawa wasichaguliwe kuwa Mawaziri.

Wakati Christina akisema hayo, wananchi wengi wa Lamadi waliozungumzia suala hilo, walisema kuwa ni vyema mawaziri wakatokana na wabunge wa kuteuliwa na Rais.

“Zile nafasi za Rais uteuzi ambazo zipo chini ya Rais ndizo ziwe za Mawaziri, siyo kuchukua wabunge ndio wawe mawaziri, ukifanya hivyo hawa jamaa wanasahau kabisa majimbo yao,” alisema na kuongeza:
“Wanakaa huko wanakusanya fedha  za kuja kuwahonga wananchi wakati wa uchaguzi ujao.”

No comments:

Post a Comment