Tuesday, November 20, 2012

MGOGO WA ARDHI KAPUNGA KWA NUKA


Majengo ya karakana katika Mradi wa Mpunga Kapunga.

Mapato yalikuwa makubwa, lakini wakaubinafsisha Mradi

HUU ni mfululizo wa Ripoti Maalum kuhusiana na mgogoro wa ardhi Kapunga wilayani Mbarali, mkoani Mbeya kama unavyoendelea kusimuliwa na Mwandishi Wetu DANIEL MBEGA, ambaye aliyefanya uchunguzi kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu. Endelea na Sehemu hii ya Saba…

MRADI uliokuwa unategemewa kuwa mkombozi wa Taifa katika suala la uzalishaji wa chakula, hasa mpunga, ulidumu kwa miaka mitano tu na baada ya hapo ukayumba na kuporomoka kabisa.
Kwa mfumo wa vigogo wa shirika kuchota kwa mashindano kwenye Mradi wa Mpunga Kapunga, haishangazi kuona hata ripoti za uzalishaji pamoja na mapato na matumizi kuonekana zinakanganya.
Katika msimu wa kwanza wa mradi huo, yaani mwaka 1990/91, eneo lililolimwa lilikuwa hekta 423. Mkanganyiko rasmi unaanzia hapa. Wakati ambapo nyaraka mbalimbali za Serikali, zikiwemo Nyaraka za Zabuni za Kuuza Shamba hilo za Juni 2004, zinaonyesha kwamba katika msimu huo jumla ya tani 1836 zilivunwa ukiwa ni wastani wa tani 4.3 kwa hekta moja, Ripoti ya Kukamilika kwa Mradi wa Mpunga Kapunga ya Benki ya Maendeleo ya Afrika inaonyesha zilivunwa tani 1,314 za mpunga.
Hii inaonyesha kuwepo na upungufu wa tani 522 za mpunga ambazo haijulikani zilikokwenda, kwani kimsingi Ripoti ya Kukamilika kwa Mradi ilitegemea zaidi taarifa kutoka serikalini, hususan kwenye Shirika la Nafco lenyewe. Ilikuwaje mpaka maofisa wa ADB wakapewa takwimu zilizo pungufu ni swali ambalo linaweza kujibiwa na wahusika wenyewe.

No comments:

Post a Comment