Thursday, November 15, 2012

HOSPITALI YA WILAYA YA BUNDA YAKIDHIRI KWA UCHAFU

Uongozi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Bunda, umeipa hospitali teule ya wilaya  hiyo siku tatu ya kuhakikisha kuwa mazingira yake yanakuwa katika hali ya usafi, vinginevyo itasimamishwa kutoa huduma kwa jamii.
Hatua hiyo imefikiwa jana na uongozi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo na kushuhudia mazingira machafu hasa vyooni na wodini huku maji machafu  yakitiririka hovyo kutoka vyooni na mahala pa kufulia kuelekea kwenye makazi ya
watu.
Wakiongea kwa nyakati tofauti hospitalini hapo, viongozi wa mamlaka hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Pastory Ncheye na Ofisa mtendaji wake Charles Machage wamesema , mazingira ya hospitali hiyo yanatia shaka kuhusu huduma  za matibabu zinazotolewa mahala hapo hivyo wameutaka uongozi wa hospitali kuyasafisha mazingira yake vinginevyo itaisimamisha kufanya kazi.
Akisisitizia hilo Ncheye amesema inatia aibu kuona kuwa hospitali ambayo inaelimisha watu namna ya kujikinga na magonjwa pamoja na kuwatibu pindi wanapougua mazingira yake ndiyo yanayoongoza kwa uchafu wenye kuchangia maambukizo ya maradhi kwa jamii jambo linalotia shaka kama kweli hospitali hiyo inawiwa na afya za watu.
“Jamii inategemea kuyaona mazingira ya hospitali katika hali ya usafi lakini kwa hapa hali ni kinyume.Sasa tunawataka muisafishe hospitali yenu ndani ya siku tatu vinginevyo tutawazuia kutoa huduma,”aliseman Ncheye.
Hata hivyo Ncheye ametilia shaka utendaji kazi wa wataalamu wa idara ya afya wenye jukumu la kuangalia hali ya usafi ndani ya mamlaka hiyo kama wanatekeleza majukumu yao vizuri kwani hawajawahi kuitolea taarifa yoyote hospitali hiyo kuhusu mazingira yake na kumwagiza ofisamtendaji wa mamlaka hiyo kuwachunguza na kuwachukulia hatua ikibainika kama walizembea katika hilo.

Kwa upande wake katibu wa hospitali hiyo, Billy Kinyaha alipoulizwa alikiri kuwepo kwa hali ya uchafu hospitalini hapo unaosababishwa na
ukata unaoikabili kutokana na Serikali kutoipatia fedha za uendeshaji kwa wakati na kusema wanajitahidi kuyasafisha kwa fedha kidogo wanazozipata kutoka katika chanzo ambacho hakukitaja na kwamba kwa sasa hali ya usafi inaendelea kuboreka.

No comments:

Post a Comment