Wednesday, October 31, 2012

TREN YAWAVUTIWA WENGI DAR



USAFIRI wa treni umeonekana kuwavutia watu wengi jijini Dar es Salaam kiasi cha kuwafanya wapande na kuzunguka kutokana na ugeni wa huduma hiyo.Mbali na hilo pia usafiri huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali tangu uanze hivi karibuni.

Meneja Uhusiano wa Shirika la Reli(TRL) Midladjy Maez, alisema abiria wengi bado wanalinganisha usafiri huo na ule wa daladala.

Maez alisema kuna abiria wanaopanda treni kabla haijafika kituo cha mwisho ili wageuke nayo kwa ajili ya kuwahi nafasi kama ilivyo kwenye daladala.

Wengi wa wasafiri wanaotumia daladala huyafuata magari hayo kwenye vituo vitatu hadi vinne kabla hayajafika mwisho wa safari kwa ajili kugeuka nayo jambo linalowalazimu kulipa nauli mara mbili.

Alisema wanafanya hivyo kutokana na usafiri kuwa wa tabu hasa nyakati za asubuhi wanapokwenda kazini na jioni wanaporudi.

Hali kama hiyo ilijitokeza juzi ambapo abiria walipanda treni hiyo kituo cha Kamata na kwenda hadi Stesheni kwa lengo la kugeuka nayo kama wanavyofanya kwenye daladala.

Maez alisema tiketi walizokata zilikuwa zinawaruhusu kuishia Stesheni na kama ni kugeuka ilibidi wakate tiketi nyingine ambapo wangelipa nauli ya Sh800.

Meneja Uhusiano huyo alisema kuwa idadi ya abiria iliyojitokeza juzi ilikuwa kubwa kuliko walivyotarajia, kiasi ambacho tiketi ziliwaishia na kusababisha wengi kusafiri bure.
Alisema ipo kamati ambayo inashughulikia na kuaangalia tatizo ili lisijitokeze tena.
Wakati usafiri huo ukiingia siku ya nne leo, ukarabati wa reli inayotoka stesheni kwenda Ubungo Maziwa unaendelea kwa lengo la kuboresha huduma hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Miliki wa Rasilimali za Reli (Rahco) Mhandisi Benhadard Tito alisema matengenezo ya awali yamekamilika kwa sasa wanaboresha tu huduma.
Mhandisi Tito alisema ujenzi wa vituo maeneo ya Ubungo Maziwa, Mwananchi, Kamata na Stesheni unakaribia kumalizika.

“Vituo tunavyojenga tunataka pia viweze kuwasaidia walemavu na wazee, si unajua ngazi za treni zilivyo ndefu” alisema.
Imeandikwa na Zacharia Osanga, Suzan Mwillo na Hadija Jumman

No comments:

Post a Comment