Mwigizaji mkongwe nchini, Bakari Mbelemba, maarufu kwa jina la
kisanii la Mzee Jangala, amesema atatumia Tamasha la Ngoma za Asili
“kutangaza nia ya kugombea urais” wa Jamhuri ya Muungano.
Tamasha hilo litafanyika Juni 13 kwenye Uwanja wa Taifa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal amealikwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na gazeti hili kwenye ofisi za gazeti
la Mwananchi jana, Mzee Jangala alisema ana haki na sifa zote za
kugombea nafasi hiyo ya juu, kama waliotangulia kutangaza nia na
kuwataka wananchi kutombeza kwa uamuzi wake.
Mzee Jangala, ambaye mara nyingi huigiza kama mzee
mbishi na mwenye kauli za vichekesho, amesema Watanzania hawana budi
kusubiri kusikia sera zake na mikakati yake endapo akifanikiwa kupata
nafasi hiyo.
“Nimepanga kutangaza nia ya kugombea urais siku
hiyo kwenye Uwanja wa Taifa mbele ya Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib
Bilal, ambaye atakuwa mgeni rasmi katika tamasha la kihistoria la ngoma
za asili,” alisema Mzee Jangala.
“Najua watu watafikiria natania katika jambo hili.
Lakini siko hivyo. Nina uhakika na ninachokisema kwani ni haki ya kila
raia na inatambulika kikatiba kugombea nafasi hii nyeti endapo tu ukiwa
unazo sifa na vigezo,” alisema Mzee Jangala.
Msanii huyo mkongwe, ambaye hakutaja atagombea kwa
chama gani, alisema kilichomsukuma kutangaza nia kwanza ni mzalendo na
mapenzi kwa nchi yake.
“Pili ni kuondoa tatizo la mmomonyoko wa maadili
kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana na wananchi,” alisema msanii
huyo aliyeanzia katika uigizaji wa jukwaani.
Alisema baadhi ya viongozi wakipewa madaraka
wanasahau walikotoka na kutenda mambo kinyume na matarajio ya wananchi.
Hali inayosababisha shughuli wanazozifanya kutofanyika ipasavyo na
kuibua minung’uniko.
“Hawa tuliowachagua, baadhi yao hawana uchungu na
nchi hii ndiyo maana rushwa imekuwa sehemu ya maisha yetu, kwa sababu
walioko madarakani wapo kwa masilahi yao binafsi na si ya Watanzania,”
alisema Mzee Jangala.
“Rushwa imekuwa changamoto mojawapo, sasa basi
mimi nina uwezo, najiamini kuongoza na kupambana na jambo hili.
Kinachohitajika kwa Watanzania kuniunga mkono pindi nitakapotangaza nia
yangu.”
Hata hivyo, Mzee Jangala hakuwa tayari kutaja
vipaumbele vyake endapo atapata nafasi ya kugombea urais akisema kuwa
bado ni mapema sana. Ukizingatia kuna wimbi kubwa la Watanzania
wanaotarajia kutangaza nia ya nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment