Sunday, December 8, 2013

RATIBA YA MAZISHI YA MANDELA



Ratiba inayoonyesha namna siku kumi za maandalizi ya mazishi ya kitaifa ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela atakayezikwa kijijini kwake Qunu, Eastern Cape, imetolewa.
Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma akizungumza na waandishi wa habari juzi, alisema kuwa Desemba 8 itakuwa siku ya sala na kukumbuka mambo aliyoyafanya Mandela.
“Tunawaomba watu wetu wote wakusanyike kwenye kumbi za mikutano, makanisa, misikiti, mahekalu, masinagogi na nyumba zao kwa ajili ya sala na kutafakari kuhusu maisha ya Madiba na mchango wake kwa taifa letu na dunia, “ alisema Zuma.
Kwa mujibu wa CNN, siku hiyo itatumiwa na viongozi wa kitamaduni kukutana, nyumbani kwa Mandela au chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya kufanya sherehe ya kimila ijulikanayo kama ‘kufumba macho.’
Viongozi hao watakuwa ‘wakiongea’ na Mandela na mababu zake wakiwaelezea namna mambo yalivyotokea katika kila hatua.
Inaaminika kuwa baada ya sherehe hiyo, mwili wa Mandela utahifadhiwa katika chumba cha maiti kwenye hospitali ya jeshi ya Pretoria.
Ibada rasmi ya kumwombea Mandela itafanyika Jumanne, Desemba 10 katika uwanja wa michezo wa FNB wenye uwezo wa kuchukua watu 95,000 uliopo Soweto, mahali ambapo Madiba alionekana hadharani kwa mara ya mwisho alipokwenda kuangalia Kombe la Dunia Julai 2010.
“Kuanzia tarehe 11 hadi 13 Desemba, mwili wa mpendwa wetu Madiba utapelekwa katika majengo ya Muungano, yaliyopo Pretoria, mahali ambako alifanya kazi kama rais wa kwanza katika demokrasia changa baada ya kuapishwa Mei 10, 1994,” alisema.
Mwili wa Mandela utawekwa kwa siku tatu katika majengo hayo ili watu waweze kutoa heshima za mwisho. Siku ya kwanza imetengwa kwa ajili ya watu mashuhuri pekee.
“Katika kipindi chote hicho, ibada za kumwombea zitakuwa zikiendelea kwenye majimbo na mikoa yote,” alisema.
Maelfu ya waombolezaji wanatarajiwa kujitokeza barabarani Desemba 14 kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mithatha kushuhudia wanajeshi wakisafirisha mwili wa Mandela kuelekea Kijiji cha Qunu, mahali atakapozikwa Desemba 15.
Mwili wa Mandela ukifikishwa kijijini kwake, utakabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya taratibu za mazishi, ambapo bendera ya taifa itaondolewa  kwenye jeneza na kufunikwa kwa blanketi la kitamaduni la Xhosa kuashiria kurudi kwa mmojawao.

No comments:

Post a Comment