Monday, December 2, 2013

POLISI WADAIWA KUWAKATA MIGUU WATOTO

Kamanda wa Mkoa wa Morogoro, Faustine ShilogileUKATILI kwa watoto wadogo nchini unazidi kushika kasi ambapo askari polisi wanne wa Kituo cha Turiani Mvomero, wanatuhumiwa kuwavunja miguu na mbavu watoto wanne kwa kuwapiga kwa madai ya kuiba vyuma chakavu.
Malalamiko hayo yalitolewa jana na wazazi wa watoto hao, Stephania John (75), Kudura Rajabu (33), wakidai watoto wao Elias Michael (11) na Dickson Kudura (15) wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Bwagala wakiwa wamefungwa bandeji ngumu (POP).
Rajabu ambaye ni mzazi wa Dickson na Stephania mama mzazi wa Elias, walisema kuwa waliambiwa kuna mtu alikwenda polisi akidai watoto hao, Elias, Dickson, Ismail Seif na Victor Elias, waliiba vyuma chakavu na vipuri vya gari, rim mbili, jeki, betri, vioo, simu tano na sh 150,000.
“Hatutetei watoto hao, kama wamefanya makosa wangestahili wakumbane na mkono wa sheria, lakini si kama polisi walivyojichukulia hatua mkononi ya kuwafanyia unyama wa kuwapiga, kuwavunja miguu na kuwapa ulemavu wa kudumu,” alisema Stephania.
Waliwataja askari wanaodaiwa kuhusika kuwatesa watoto wao kuwa ni Afande Muddy (Traffic), Robert, Romano’s na askari mgambo aitwaye Gogo.
Walipoulizwa wanachukua hatua gani, walisema wao ni watu duni, hawana uwezo wa kifedha.
“Kila njia tumefanya tangu Novemba 17 mwaka huu, tumeishia kupigwa ‘changa la macho’, tumesikia askari wamewekwa ndani, lakini tunanong’onezwa usiku wanalala makwao, labda taasisi za haki za binadamu zitusaidie,” alisema Stephania.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Turiani, Fineous Majura alipohojiwa hakuonyesha ushirikiano akidai kuwa si msemaji bali atafutwe Kamanda wa Mkoa, Faustine Shilogile.
Wazazi hao wamegoma kuwachukua watoto wao hospitalini wakiitaka polisi walipe gharama za kuwatoa kama walivyolipa gharama za kiingilio cha matibabu na kisha wawapeleke mahakamani ili wakawawekee dhamana huko.

No comments:

Post a Comment