SIMBA
imemtumia tiketi ya ndege kipa wa zamani wa Yanga, Yaw Berko na atatua
jijini Dar es Salaam kesho Ijumaa kufanya mazungumzo ya mwisho na klabu
hiyo ya Msimbazi.
Mwanaspoti linaweza kuthibitisha
pasipo shaka kuwa Berko atatua kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Kenya
kwa ajili ya kufanya makubaliano ya kuidakia Simba kuanzia mzunguko wa
pili wa Ligi Kuu Bara unaoanza Januari 25 mwakani.
Simba imepanga kumpa mkataba wa miezi
sita Berko ambao utakwisha Juni mwakani na kuwepo kwake kutategemeana na
kanuni mpya za Ligi Kuu Bara kwani huenda kusiwe na makipa wa kigeni
kuanzia msimu ujao kama kanuni mpya zitaanza kutumika.
Tayari uongozi wa Simba umempa maagizo
kipa wao wa sasa raia wa Uganda, Abel Dhaira kumtaka atafute timu
nyingine kutokana na kupungua kiwango pamoja na gharama kubwa.
Mmoja wa waandishi maarufu wa Ghana
aliliambia Mwanaspoti jana Jumatano kuwa Berko amepokea tiketi hiyo na
atatua katika ardhi ya Tanzania Ijumaa.(P.T)
Berko alipopigiwa simu kuthibitisha
habari hizo, kwanza aliguna, halafu akazungumza kwa Kiswahili; "Wewe
nani? Baada ya mwandishi kujitambulisha na kumuuliza kuhusu suala la
kujiunga Simba alicheka halafu akasema: ''Nipigie baadaye tuzungumze
nipo mazoezini." Hata hivyo hakupatikana tena.
Viongozi wa Simba walionekana kushangazwa kila walipotafutwa kuthibitisha hilo, huku wengi wakisema hawana habari na hilo.
Hata hivyo, uchunguzi wa ndani wa
Mwanaspoti unaonyesha kuwa Berko ameipokea tiketi ya ndege aliyotumiwa
na Simba na atatua kesho Ijumaa kufanya mazungumzo na klabu hiyo ya
Msimbazi.
Berko aliondoka Yanga mwaka huu baada
ya klabu hiyo ya Jangwani kumpa dola 7,500 (Sh 12 milioni) alizokuwa
anawadai kutokana na kuvunja mkataba.
Yanga ilimtoa Berko kwa mkopo kwenda
FC Lipopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili wabadilishane na
Mnyarwanda Kabange Twite, pacha wa kiraka wa klabu hiyo, Mbuyu Twite,
lakini mpango huo ulishindikana msimu uliopita.
Baadaye kipa huyo bora wa Ligi Kuu
Bara msimu wa mwaka 2011/12 alibaki Jangwani lakini bila kucheza akawa
mtu wa kujifungia chumbani muda wote makao makuu ya Yanga.
Berko, ambaye matarajio yake ya mbele
ni kuwa mchungaji wa kanisa alipokuwa anawaaga mashabiki wa Yanga mapema
mwaka huu, alisema anaondoka Jangwani, lakini kuna siku watamkumbuka.
"Nimefanya kazi vizuri na Yanga na
sasa narudi nyumbani kufanya mambo mengine, nitawakumbuka sana, na Yanga
najua watanikumbuka sana," alisema Berko alipokuwa anaondoka.
Akiwa Yanga, Berko anakumbukwa kuwa
kipa imara klabuni hapo na akawa kipa bora wa ligi msimu wa 2010/2011,
ingawa nyota yake ilififia alipokuwa na majeruhi ya bega yaliyokuwa
yanamweka benchi mara kwa mara hali ambayo ilizua utata kuwa alikuwa
anafanya makusudi.
Berko alijiunga na Yanga mwaka 2009,
akitokea Liberty Proffessional ya kwao Ghana, timu ambayo ilimuibua pia
Michael Essein na nyota wengine kibao wa Ghana. Aliletwa nchini na kocha
wa zamani wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic aliyewahi kufundisha katika
klabu ya Hearts of Oak ya huko.
Berko anajivunia kuiwezesha timu
kutwaa mataji ya ubingwa wa Bara msimu wa 2010/2011 na Kombe la Kagame
mara mbili mfululizo; 2011 na 2012.
Mwaka 2011 alidaka mechi zote Kombe la
Kagame, lakini 2012 alidaka hadi robo fainali alipoumia na kumuachia
Ally Mustafa 'Barthez' aliyedaka hadi ubingwa.
Chanzo:Mwanasport mtandaoni
No comments:
Post a Comment