SIKU moja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kumfutia kesi raia wa Kenya, Joshua Mulundi, ya kuteka na kujaribu kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, Jeshi la Polisi limeanza sarakasi mpya za kutupiana mpira.
Wakati polisi wakikwepa kuwataja wahusika wa tukio hilo, wadau wamedai kuwa vyombo vya dola vinamkumbatia mmoja wa maofisa wa usalama aliyetajwa na Ulimboka kuhusika na utekaji huo.
Itakumbukwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliunda jopo la maaofisa kutoka kanda hiyo na makao makuu kuchunguza tukio hilo na kutamba kuwa halitatokea tena.
Licha ya tambo hizo, hadi sasa jopo hilo halijawahi kutoa hadharani ripoti ya kile walichokibaini hadi tukio jingine kama hilo likajirudia Machi 6, mwaka huu, alipotekwa na kuteswa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini, Absalom Kibanda.
Watuhumiwa wa tukio la Kibanda pia hawajakamatwa pamoja na Kova kuunda jopo la uchunguzi.
Alipotafutwa jana kuzungumzia uamuzi wa DPP kumwachia huru Mulundi kutokana na kutopatikana ushahidi wa kumtia hatiani kutenda kosa hilo, Kova aligoma katakata kutaja kile kilichobainiwa na jopo la kamati yake ya uchunguzi.
Badala yake Kamanda Kova alisema suala hilo lilikwisha kuondoka kwao na kwamba yeyote anayetaka kujua undani wake ni vema akajaribu kuwasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba.
Kova alisema masuala yote hayo ikiwamo watuhumiwa kudaiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi hayako kwake.
“Kwanza uliwahi kunisikia hata siku moja nikimuita mtuhumiwa gaidi, sijawahi, mimi kazi yangu ni kukamata wahalifu mbalimbali wakiwamo wa magari kama haya niliyowaonyesha baada ya kuibwa na majambazi wanaotumia silaha,” alisema Kova.
Tanzania Daima lilimtafuta Kamishna Manumba ili kupata undani wa hatua inayofuata baada ya mtuhumiwa pekee kuachiwa, lakini ofisa huyo naye alikuwa na majibu ya kukwepa.
“Hivi baada ya kuachiwa kilitokea nini? Si umeona alikamatwa tena?” alihoji Manumba ingawa alipobanwa kuwa hakukamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka, alisema sheria inasema kuwa mtu yeyote anaposema uongo, moja kwa moja atakuwa ametenda kosa.
Aidha, alipotakiwa kutolea maelezo mtindo uliozuka wa watu kubambikiziwa kesi za ugaidi, kamishna huyo hakutaka kusikiliza, zaidi ya kusema: “Kwa heri,” kisha kukata simu yake.
Wadau wahoji
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wadau hao walionyesha hofu kwamba kwa sasa kuna hatari ya wananchi kubambikizwa kesi za baadhi ya watu serikalini wanaofanya vitendo hivyo bila kuchukuliwa hatua zozote.
Mkurugenzi wa zamani wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya, alieleza kusikitishwa na kitendo cha polisi kutomtia hatiani ofisa wa Ikulu aliyetajwa kwa jina la Ramadhani Ighondu, kuwa ndiye aliyeratibu tukio hilo la kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka.
“Kesi ya Dk. Ulimboka mbona ipo wazi, mtuhumiwa yupo wazi, alitajwa na aliyeteswa, serikali ndiyo imemlinda. Kwa hali hii tunakuwa na hofu kuwa vyombo vyetu vya usalama vinatesa watu na kuwalinda watesaji,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa ni kama vile kuna vyombo vya ulinzi vya watu wachache. Kwamba, Tanzania sasa si salama, hakuna utawala bora, haki za binadamu hazizingatiwi wala hakuna demokrasia na uhuru wa mawazo.
Hili si jambo la kuchekea, ni suala la kulaaniwa na kuhuzunisha kwa kila Mtanzania. Ni aibu sana tunapokuwa na serikali inayotesa watu wake,” alisema.
Nkya aliongeza kuwa kwa hali hii Rais Jakaya Kikwete afafanue hadharani kwa Watanzania kuhusu tukio hilo, vinginevyo haeleweki vizuri.
Naye Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema uamuzi wa DPP kuwasilisha mahakamani hati ya kutoendelea na mashtaka hayo ni ishara ya wazi kuwa aliona hayana msingi.
Alisema kuwa mashtaka hayo yalifunguliwa kutumia kisingizio cha kesi kuwa mahakamani ili kudhibiti vyombo vya habari visiandike habari za uchunguzi kuhusu kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka.
Mnyika pia alifafanua kuwa ilikuwa ni njia ya kuzuia Bunge lisijadili na kuihoji serikali. “Uamuzi huu wa DPP sasa umefungua mlango kwa vyombo vya habari kuandika na wabunge kujadili, kwani mmoja wa watuhumiwa ni ofisa wa Usalama wa Ikulu,” alisema.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa kwa uamuzi huo, Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda Kova wajitokeze waseme kuwa walilidanganya taifa kwa mwaka mzima, na kwamba sasa wawaeleze Watanzania nani hasa alimteka na kumtesa Dk. Ulimboka.
No comments:
Post a Comment