Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema baadhi ya wabunge wa CCM ni mizigo kwani hata wakienda bungeni, hawachangii na wanabebwa na chama.
Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa,
alisema hayo juzi jioni kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
Uwanja wa Shule ya Msingi Nyamikoma, Kata ya Busega Mkoa wa Simiyu ikiwa
ni sehemu ya kampeni za kuimarisha uhai wa chama.
“Ukweli ni kwamba, baadhi ya wabunge wa jinsi hii
hawatufai. Wanakwenda bungeni hawachangii, wanakwenda bungeni hawana
hata hoja za kuchachafya upinzani, hawachangii, hawa ni mzigo,” alisema
Sitta.
Sitta alisema licha ya aina hiyo ya wabunge, pia wapo wale ambao hawafiki majimboni kwao kukagua shughuli za maendeleo.
“Wapo baadhi ya wabunge, hawajawahi hata siku moja
kwenda kwenye majimbo yao kuwatembelea wananchi waliowachagua...
inawezekana hata wapiga kura wakawa wamewasahau. Hawa hawafai hata
kuchaguliwa wakiomba tena kura,” alisema na kuongeza:
“Haiwezekani mbunge akakaa mjini na kushindwa
kwenda kuwatembelea watu wake jimboni. Mbunge anakwenda jimboni kwa
kuchungulia halafu wananchi wanamshabikia na kumpa kura?
“Rais Jakaya Kikwete amejitahidi sana kuleta
mabadiliko, ameleta mafanikio ya uchumi na mambo mengi. Inatakiwa
wabunge waende wakawaeleze wananchi maendeleo haya, inawezekana
hawayajui lakini watu hawaendi majimboni, wananchi watayafahamu vipi
haya maendeleo?”
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya, Sitta
alisema: “Kwanza kuna viashiria vya baadhi ya watu kuanza kuipinga
Katiba mahakamani. Watu hao wasiungwe mkono kwani ndio wanaoanza
chokochoko.
“Katiba tunayoitaka ni kwa ajili ya maendeleo ya
Tanzania na Watanzania na si ya wengine. Hivyo hatuna budi kila mmoja
kutumia nafasi hiyo kuwasilisha mchango wake wa kuboresha kwenye
Mabaraza ya Katiba.”
Aliwataka wajumbe wa Mabaraza ya Katiba watumie
nafasi kuwasilisha hoja zinazojenga na wasiwe mamluki wa kuharibu
mchakato mzima.
Awali, Sitta alishiriki katika harambee ya
kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki la Kiloleli, Wilaya ya Busega na
kuchangia Sh3 milioni.
Akizungumza katika harambee hiyo, iliyotarajiwa
kukusanya Sh217,538,000, Sitta aliwataka wazazi kuwalea watoto wao
katika misingi ya dini ambayo baadaye hutoa viongozi bora na wenye
maadili... “Huwezi kuchukua tu mtu awe kiongozi, lazima wafunzwe misingi
ya maisha na uongozi.”
No comments:
Post a Comment