Sunday, June 2, 2013

MWENYEKITI WA CHADEMA AKIMBILIA CCM

Kampeni za udiwani katika kata nne jijini Arusha zimezidi kushika kasi mara baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema kata ya Elerai,Dominick Mboya pamoja na makada mbalimbali wa chama hicho juzi kutangaza kuhamia CCM.
Makada hao walitangaza uamuzi wao wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika kata ya Kaloleni ambapo kwa pamoja walipanda kwenye majukwaa ya kampeni na kisha kukabidhiwa kadi za kujiunga na chama hicho.
 
Akitangaza uamuzi wa kuhamia Chadema mbele ya menyekiti wa jumuiya ya wazazi wa CCM taifa,Abdallah Bulembo ambaye alikuwa mgeni rasmi  ,Mboya alisema kwamba ameamua kuhamia CCM baada ya kubaini kwamba Chadema kinaendeshwa kibabe.
Alisema kuwa msimamo wake wa kutotaka kuburuzwa ndani ya Chadema ndiyo umemsukuma kuhamia CCM na kusisitiza ya kuwa nyuma yake ameacha zaidi ya makada 200 wa Chadema ndani ya kata ya Elerai ambao wako njiani kumfuata.

Hatahivyo,aliibua madai mazito katika mkutano huo ambapo alisema kwamba wakati akiwa Chadema yeye pamoja na baadhi ya viongozi bila kutaja majina yao hadharani kwamba walikuwa wakisuka njama kila kukicha za kuandaa maandamano mbalimbali kama mgomo wa daladala bila sababu za msingi.
Akiwapokea makada hao Bulembo alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kutumia udini na ukabila katika kujipatia kura kutoka kwa wananchi na kutaka ikomeshwe mara moja.
Bulembo,alisema kwamba hoja ya udini haina mashiko katika kipindi hiki cha kampeni na kumtaka mgombea wa udiwani ndani ya kata hiyo kukemea suala hilo katika majukwaa atakayopanda.
Mgombea wa udiwani wa kata hiyo,Emmanuel Milliari kwa upande wake aliwaomba wakazi wa Kaloleni kumchagua kwa kishindo kwa kuwa yuko tayari na ana uwezo wa kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Alisema pindi watakapomchagua atajikita kutatua kero ya michango kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ndani ya kata hiyo sanjari na kero ya uchafu wa taka unaoikabili kata ya Kaloleni.

No comments:

Post a Comment