Monday, June 17, 2013

MASIKINI MTOTO HUYU JAMANI



Kagera. “Jinsi nilivyoangaika na mtoto huyu najisikia kukata tamaa ila sina jinsi, naomba tu Mungu anisaidie aniongezee moyo wa uvumilivu na subira hadi atakapopona,” hii ni kauli ya Juster Vedasto (26) mkazi wa eneo la Kamizilente Kata ya Rwamishenye katika manispaa ya Bukoba, ambaye mtoto wake amevimba kichwa kwa zaidi ya miaka mitatu sasa kutokana na kujaa maji.
Mtoto huyo Anitha Alex mwenye umri wa miaka mitatu na miezi kumi na mmoja alipatwa na tatizo hilo la kuvimba kichwa akiwa na umri wa miezi mitatu, kwa mujibu wa mama yake, alianza kuvimba sehemu za utosini na baadae kichwa kizima.
Mtoto huyo ambaye mwaka jana kupitia vyombo vya habari aliomba kupatiwa msaada kwa ajili ya kwenda Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro kupatiwa matibabu ya kichwa, bado anahitaji kusaidiwa ili aendelee na matibabu.
Kwa mujibu wa mama yake, msaada aliopatiwa mwaka jana ulimwezesha kwenda katika hospitali hiyo na kufanyiwa upasuaji wa kichwa Juni 5, 2012 aliwekewa mpira kwa ajili ya kutoa maji kichwani.
Juster anasema mtoto wake alitakiwa kurudishwa katika hospitali hiyo Februari 15 mwaka huu kwa ajili ya kubadilishiwa mpira aliowekewa kichwani, lakini hana hata nauli, achilia mbali gharama za matibabu.
“Nilipofika Moshi mwaka jana nilipata msamaria mwema aitwaye Benedicto Tarimo ambaye alinipa makazi na huduma zote muhimu na sasa nikipata nauli nategemea niende kumwomba tena msaada kama alionipa mwaka jana, kwa sasa sina mawasiliano naye baada ya simu yangu kuibiwa” anasema Juster.
Mtoto huyo ambaye anakaribia umri wa miaka minne sasa bado hajaweza kusimama wala kutembea ambapo pia Februari 18 mwaka huu alitakiwa kupelekwa katika kitengo cha mazoezi kilichoko katika hospitali hiyo ili aanze kufanyishwa mazoezi ya kusimama.
“Tangu alipofanyiwa upasuaji wa kwanza naona kuna mabadiliko, sasa naona shingo imekaza ilikuwa inalegea, ameanza kukaa mwenyewe wakati kabla ya upasuaji alikuwa analala muda wote asingeweza kukaa, nina imani atapona naomba Watanzania wasinichoke.
Juster anasema hana uwezo wa kufungua akaunti katika benki na kuwa akiifungua hana uwezo wa kupata fedha za kuweka hivyo anawaomba wanaohitaji kumsaidia watumie namba yake ya simu ambayo ni 0765230488 hata kwa kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi.

No comments:

Post a Comment