Sunday, June 9, 2013

MAHANGA AJIHAMI KUELEKEA UCHAGUZI 2015

 Mbunge wa Segerea, mkoani Dar es Salaam, Makongoro Mahanga amewaonya makada wa CCM walioanza kujipitisha kutaka kugombea ubunge katika jimbo hilo mwaka 2015 kwamba muda wa kufanya hivyo, kwa mujibu wa taratibu na kanuni za chama hicho bado haujafika.
Aidha alisema yeye bado anatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hadi 2015 na watu wanaoanza kampeni sasa hivi wanavuruga mipango yake ya kutekeleza ahadi zake akishirikiana na wana CCM na wananchi kwani kampeni hizo zitaanza kuleta makundi yanayoweza kukwamisha kazi zake za ubunge.
Dk Mahanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira alikuwa akizungumza kwenye mikutano na viongozi na wanachama wa CCM na wananchi kwa nyakati tofauti katika Kata za Segerea, Kinyerezi na Tabata mwishoni mwa wiki.
Aliwakumbusha wana CCM kwamba yeye aliomba ubunge kwa miaka mitano na si miaka mitatu, hivyo wamwache atekeleze majukumu yake kwa ufanisi hadi mwaka 2015.
DK Mahanga aliongeza kusema kwamba itakapofika mwaka 2015 na chama kikisharuhusu, anawakaribisha wagombea wote wanaotaka ubunge wa Segerea kuchukua fomu na kuanza kampeni, lakini siyo sasa.
“Wanaotaka kupambana na mimi mwaka 2015 kwa sasa waniache nitekeleze Ilani, waje 2015 tupambane, lakini wajiandae vizuri kwani mimi hapa Segerea bado nipo nipo sana. Na wasiojua vita vyangu wafikirie mara mbili kabla hawajachukua fomu,” alionya Dk Mahanga.
Alidai kwamba jeuri na kujiamini kwake kunatokana na ukweli kwamba anatekeleza vizuri Ilani ya Uchaguzi ya CCM na ikifika mwaka 2015, wananchi wa Segerea watafurahia kazi yake.
Akitolea mifano ya utekelezaji wa Ilani kwenye jimbo lake, kwa upande wa barabara alisema licha ya baadhi ya barabara kukamilika kujengwa kwa lami kama Kimanga – Mazda, barabara ya Uhuru Malapa – Mandela, na St Mary Tabata, alielezea ujenzi wa barabara ya Vingunguti – Baracuda, Kinyerezi – Kifuru, na Tabata Dampo – Kigogo ambazo zitaanza kujengwa kwa lami kuanzia mwezi ujao. Pia alitaja barabara za Baracuda – Chang’ombe – Mazda, Segerea Oilcom – Majumba Sita, na Segerea – Bonyokwa – Kimara ambazo pia ziko kwenye mpango wa kujengwa katika mwaka wa fedha 2013/14.
Kwa upande wa kero ya maji alisema kuanzia mwishoni mwa mwaka 2014 hadi mwanzoni mwa 2015, kero ya maji katika jimbo hilo itakuwa imekwisha baada ya mradi wa ujenzi wa mtambo wa Maji wa Ruvu Juu na usambazaji wa maji kukamilika. Hata hivyo kwa sasa visima kadhaa vinaendelea kuchimbwa katika maeneo mbalimbali kusaidia upatikanaji wa maji.

No comments:

Post a Comment