Tuesday, June 11, 2013

MADAKTARI WA MISRI KUENDESHA OPERESHENI BILA UPASUAJI MUHIMBILI

 
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi
Madaktari bingwa wanane kutoka nchini Misri wataota huduma ya operesheni ya kisasa inayofanywa bila upasuaji sehemu ya tumbo itakayofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN), jijini Dar es Salaam.

Operesheni hiyo ya siku tano itakuwa tofauti na ile iliyozoeleka ya kupasua sehemu kubwa ya mwili.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa madakitari hao watatoa huduma kwa watu wote watakaoenda katika MNH na kugundulika kama wana matatizo yanayohitaji upasuaji.

Alisema licha ya kutoa huduma hiyo, madaktari hao pia watatoa mafunzo kwa madaktari wa MNH wa vitengo vya upasuaji.

Kwa mujibu wa Waziri Mwinyi, siyo mara ya kwanza kwa madaktari hao kuja nchini kutoa huduma za afya na kwamba, wapo wengine wanatoa huduma kama hizo Unguja na Pemba, visiwani Zanzibar.

Alimshukuru Balozi wa Misri nchini, Hossam Omar, kwa ushirikiano, ambao nchi yake imekuwa ikiutoa katika nyanja mbalimbali, hasa zinazohusu masuala ya afya.

Naye Balozi Hossam alisema serikali yake itaendelea kutoa wataalamu ili kushirikiana ujuzi na kutoa huduma kwa Watanzania wenye matatizo ya afya.

Alisema huu ni mwanzo mzuri wa ushirikiano, ambao lengo lake ni kuhakikisha sekta ya afya nchini inaimarika.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment