Saturday, June 8, 2013

Kwa rasimu hii, CCM ijiandae kutoka kwenye fungate


Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Katiba inatarajia kuleta Katiba yenye mwelekeo mpya kabisa kwa taifa letu.
Rasimu hiyo imependekeza mambo mbalimbali ikiwamo mabadiliko katika muundo wa Serikali ambapo imependekeza kuwepo kwa Serikali tatu katika Muungano, muundo wa Bunge, uchaguzi wa rais, mgombea binafsi, Tume ya Uchaguzi, Baraza la Mawaziri, Mahakama, Spika na Naibu wake.
Katika mjadala wangu leo, nitajaribu kurejea historia ya taifa letu kwa kuzingatia kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndicho chama tawala tangu tupate uhuru.
CCM ni matokeo ya kuungana kwa TANU na ASP mwaka 1977. Kabla ya muungano huo, TANU kwa upande wa Tanzania Bara chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere kilijijenga kama chama dola, baada ya kushika hatamu za uongozi mwaka 1965.
Hapo ndipo chama kikawa Alpha na Omega. Mfumo wa vyama vingi ukafutwa, asasi za kiraia zikadhoofishwa na uhuru wa habari ukasiginwa.
Kimsingi Tanzania wakati huo ilikandamiza mfumo wa demokrasia kwani waliopata nafasi ya uongozi na fursa nyingine walikuwa ni viongozi wachache.
Hata ilipofika mwaka 1977 wakati wa kuzaliwa kwa CCM, bado chama kikaendelea kuwa kimoja chenye mabavu yote. Hata katiba iliyodumu hadi leo ina mwelekeo wa chama kimoja tu.
Mwaka 1992 wakati wa kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya Maoni kuhusu Mfumo wa Vyama vingi, Jaji Francis Nyalali licha ya kuleta maoni hayo, alipendekeza kufutwa kwa sheria mbovu 40 ili kujenga mazingira bora ya mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo, sheria hizo hazikufutwa na Katiba iliyokuwepo haikuandikwa upya ili kufuata mwelekeo wa vyama vingi.
Hivyo tuliingia kwenye mfumo wa vyama vingi katika mazingira magumu yasiyoleta ushindani sawa kati ya vyama hivyo.
Haikushanishagaza kuona CCM iliendelea kushinda kwa kishindo kwani, Rais ambaye ndiye mwenyekiti wa chama ameendelea kuwa madaraka ya kuteua viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama, wakuu wa mikoa na wilaya na idara nyinginezo nyeti. CCM iliweza kutumia hata majeshi ya ulinzi na usalama kutetea ushindi wake pale ilipoonekana hatari ya kushindwa.
Mbali na madaraka, CCM ilirithi rasilimali za kiuchumi, hivyo kujiweza kufanya siasa zake bila kutetereka kiuchumi.
Kwa upande mwingine, vyama vya upinzani vilikuwa bado vichanga na havikujimudu kiuchumi, hivyo ni wazi visingeweza kushindana.

No comments:

Post a Comment