Thursday, January 17, 2013

POLISI WAMJIBU SLAA


 
 
 
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa
Jeshi la Polisi nchini limesema halina mpango wowote wa kufanya njama za kumdhuru au kumuua Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.
 Dk. Slaa anadai kuwa vyombo vya usalama nchini likiwamo Jeshi la Polisi vinapanga njama za kumdhuru na kwamba amekuwa akipokea vitisho.

Kauli hiyo imetolewa jana na Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, wakati akizungumza na NIPASHE kufuatia kauli ya Dk. Slaa aliyoitoa Jumatatu na Jumanne wiki hii katika mikutano ya hadhara mkoani Kilimanjaro.


Senso alisema madai ya Dk. Slaa ya kwamba anatishiwa kuuawa halipo kama ingekuwa hivyo, hata mikutano yake anayoifanya mkoani Kilimanjaro asingeifanya.


“Kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao na si kumfanya mtu asifanye shughuli zake, wanashindwa kulala kwa ajili ya kuwalinda, shughuli zao zote wanafanya kwa sababu polisi wanawalinda na hata Dk. Slaa anafanya mikutano ya hadhara kwa sababu ulinzi upo, hivyo suala la kumtishia halipo kabisa,” alisema Senso na kuongeza:


“Kazi ya msingi ya polisi ni kuzuia uhalifu na kulinda usalama ili kuhakikisha watu wanaendelea na shughuli zao, itakuwaje waache kazi yao waanze kumwinda mtu, hata kama  wakisema wakuwinde  hivi unaweza ukatembea na kufanya shughuli zako kweli.”


Senso alisema badala ya wananchi kulaumu polisi, ni vema wakawasaidia kutoa taarifa na kushirikiana nao katika kuwabaini wahalifu hao.


Pia alisema ni bora Dk. Slaa akawaambia ukweli wananchi kuhusu namna ya kufichua wahalifu kuliko kulishutumu Jeshi la Polisi.


“Dk. Slaa kama kiongozi mkubwa wa siasa tunamuomba badala ya kulishutumu Jeshi la Polisi kwa wananchi tunaomba awaeleze ukweli na kuwaelimisha namna wanavyoweza kushirikiana nalo kuwabaini wahalifu kwani kufanya hivyo atakuwa anajenga,” alisema na kuongeza:


“Wananchi wote ambao ni raia wema wawe ni wanasiasa, walimu, wakulima na wengine wakishirikiana na Jeshi la Polisi bila kuendelea kulilaumu tutafanikiwa, tunaomba ushirikiano nao.”


NIPASHE ilipouliza kama kuna taarifa zozote za malalamiko ya vitisho ambazo ziliwahi kutolewa na Dk. Slaa kwa Jeshi la Polisi kuhusiana na madai hayo, Senso alisema hakuna na endapo angekuwa ameziwasilisha, zingefanyiwa kazi.


“Vyombo vya usalama vipo kwa ajili ya kila raia na havibagui, kama taarifa zingetolewa zingefanyiwa kazi,” alisisitiza.


Akihutubia katika mikutano ya hadhara katika uwanja wa Railway, katika Manispaa ya Moshi Jumatatu na Jumanne katika uwanja wa Kwasa Kwasa mjini Same, Dk. Slaa alisema amekuwa akitishiwa kuuawa kwa zaidi ya mara tatu huku akisisitiza kwamba hadi sasa wahusika wanaendelea na mipango hiyo na kwamba Chadema imeibaini.


“Bahati mbaya mipango inayopangwa imekuwa ikivuja kwa kuwa nyumba yao inavuja na hivyo wenye uchungu na nchi wamekuwa wakitoa taarifa hizo, sitaacha siasa kwa vitisho vya vyao na ndiyo kwanza nasonga mbele nimejitoa maisha yangu,” alisema.


Pia alililaumu jeshi hilo kwamba linaminya demokrasia huku akitoa mfano kwamba jeshi hilo Januari 14, mwaka huu liliwazuia vijana wa Manispaa ya Moshi  kutundika bendera za Chadema katika pikipiki na kurudia kitendo hicho juzi kwa vijana katika mji wa Same.


Aidha, Dk. Slaa alipoulizwa na NIPASHE juzi mjini Same kama amewahi kuripoti matukio ya vitisho dhidi yake kwa vyombo vya dola, alisema hatakwenda katika chombo chochote cha dola kwa kuwa hao hao ndio wanaotaka kumdhuru.


Alisisitiza kwamba hataacha siasa kutokana na vitisho hivyo na kwamba yupo tayari kufa kwa ajili ya kutetea umma na Watanzania katika kupata haki yao ikiwamo kunufaika rasilimali zao ambazo alisema zinanufaisha watu wachache.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment