Saturday, December 22, 2012

WANAFUNZI 2,700 WAKOSA SHULE MOROGORO


JUMLA ya wanafunzi 2,700 waliomaliza elimu ya msingi wamekosa nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari kwa mwaka 2013 mkoani Morogoro kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa 68.

Katibu Tawala wa mkoa Morogoro, Eliya Mtandu alisema hayo jana wakati wa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013.
Alisema kuwa wilaya ya Kilombero na manispaa ndizo zinahitajika kufanya juhudi za ziada kutokana na kuwa na upungufu mkubwa ikilinganisha na halmashauri zingine kwani hadi sasa inahitaji vyumba 865 wakati manispaa inahitajika vyumba 754.

Mtandu aliongeza kuwa wilaya ya Ulanga ina uhaba wa vyumba 420, Kilosa (354), Mvomero (297) na hivyo kuzitaka halmashauri zote mkoani hapa kuhakikisha vyumba hivyo vinakamilika kabla ya Januari 15, 2013 ili wanafunzi hao waliokosa nafasi waweze kuingia pamoja na wenzao.

Naye Ofisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro, Wariambora Nkya, alisema kuwa jumla ya wanafunzi 27,798 wamefaulu mtihani huo sawa na asilimia 61 ya ufaulu kati ya wanafunzi 45,773 waliofanya mtihani huo.

Alisema kuwa kwa mkoa wa Morogoro wasichana ndio walioongoza kwa kufaulu wakiwa 13,994 na wavulana 13,804.

Alisema kuwa hata kimkoa msichana kutoka Shule ya Msingi Uhuru, Salma Omary Juma, ndiye ameongoza katika matokeo hayo.

Hata hivyo, alisema utoro ni miongoni mwa sababu kubwa zinazoongoza kwa kuwa na wanafunzi watoro 1327, mimba (22), hata hivyo idadi hiyo imeonekana kupungua ikilinganishwa na mwaka jana.

No comments:

Post a Comment