Beatrice Moses na Ibrahim Yamola
SERIKALI imetangaza matokeo ya
darasa la saba mwaka huu, huku takwimu za matokeo hayo zikionyesha kuwa
zaidi ya nusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza
mwaka 2013 ni wale waliopata asilimia 40 ya alama kwenda chini katika
matokeo hayo.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa wananfunzi 294,833
sawa na asilimia asilimia 52.58 waliopata daraja ‘D’ wamechaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza.
Hao wanaungana na wenzao 265,873
waliopata madaraja ya A,B na C ambao ni sawa na asilimia 47.41. Kwa
mujibu wa taratibu za mitihani ya darasa la saba, jumla ya alama zote ni
250 ambazo zimegawanywa katika madaraja matano ambayo ni A mpaka E.
Mchanganuo
wa madaraja hayo ni alama 201 hadi 250 kwa daraja la A, alama 151 – 200
kwa daraja B, alama 101 hadi 150 kwa daraja C, alama 51 – 100 kwa
daraja D na alama 0 – 50 kwa daraja E.
Waziri Kawambwa alisema
wanafunzi 560,706 walichaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari kati ya
865,534 waliofanya mtihani huo wa siku mbili; Septemba 19 na 20 mwaka
huu na kwamba mwaka huu wasichana wamefanya vizuri katika mtihani huo
kuliko wavulana.
“Wasichana waliofaulu ni 281,460 sawa na
asilimia 50.20 ya wanafunzi 560,706 wakati wavulana waliofaulu ni
279,246 sawa na asilimia 49.80,” alisema Kawambwa alipokuwa akitangaza
matokeo hayo na kuongeza:
“Matokeo yanaonyesha kuwa jumla ya
wahitimu 3,087 walipata daraja A, wakati 40,683 walipata daraja la B.
Wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja C wakati 526,397 walipata
daraja D. Watahiniwa waliobaki 73,264 walipata E”.
Takwimu
zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato
cha kwanza mwaka 2013, imeongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na
wanafunzi 515,187 waliochaguliwa mwaka jana.
“Mtihani wa
mwaka huu, kwa mara ya kwanza watahiniwa walifanya kwa kutumia
teknolojia mpya ya Optical Mark Reader (OMR) na ulisahihishwa kwa
kutumia kompyuta,” alisema.
Alisema matokeo haya yanaonyesha alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana.
Kabla
ya matokeo, wasichana waliofanya mtihani walikuwa 456,082 sawa na
asilimia 52.68 na wavulana ni 409,745 sawa na asilimia 47.32,” alisema
Dk Kawambwa.
“Watahiniwa 29,012 sawa na asiliamia 3.24
hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, vifo
na ugonjwa,” alisema.
Dk Kawambwa alisema, kati yao, ambao
hawakufanya mtihani wasichana walikuwa 12,501 sawa na asilimia 2.67 na
wavulana ni 16,511 sawa na asilimia 3.87.
Waziri huyo alisema,
udanganyifu katika mitihani kwa mwaka huu umepungua kwa kiasi kikubwa
ikilinganishwa na idadi ya mwaka jana.
“Waliofutiwa matokeo mwaka
huu ni watahiniwa 293 ikilinganishwa na watahiniwa 9,736 waliofutiwa
matokeo yao kwa udanganyifu mwaka jana,” alisema Dk Kawambwa.
Hata
hivyo, itakumbukwa serikali ilionya mwaka jana kuwa mwanafunzi
atakayebainika kujiunga na kidato cha kwanza bila kumudu stadi hizo,
Mwalimu Mkuu wa shule alikotokea mwanafunzi huyo na Msimamizi wa Mtihani
wakumaliza elimu ya msingi watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Katika
mkutano huo wa jana na Waandishi wa Habari, Dk Kawambwa hakutaja
viwango vya ufaulu kwa kila somo kama ambavyo imezoeleka katika mitihani
iliyotangulia wala mkoa uliofanya vizuri au vibaya.
Kumbukumbu
zinaonyesha kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip
Mulugo alipotangaza matokeo ya mwaka jana aliweka wazi viwango vya
ufaulu wa masomo ya Kiingereza, Sayansi na Hisabati, ikilinganishwa na
mwaka juzi.
Mulugo alisema viwango hivyo vilikuwa vimepanda kwa
mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2010 ambavyo ni Kiingereza kutoka
asilimia 36.47 hadi asilimia 46.70, Sayansi asilimia 61.33 kutoka
asilimia 56.05 na Hesabu asilimia 39.36 kutoka asilimia 24.70.
Waziri
Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo akizungumzia matokeo
hayo jana alisema: “Hili janga, kwa sababu ukifanya uchambuzi wa haraka
utabaini kuwa wanafunzi waliopata alama za daraja la A ni asilimia 0.35
tu”.
Lyimo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), alisema upo
uwezekano mkubwa kukawa na idadi kubwa ya wanafunzi wasiojiweza
waliochaguliwa kwenda Sekondari, hivyo akashauri iandaliwe program
maalum ya kuwawezesha wanafunzi hao kumudu masomo ya kidato cha kwanza.
“Kama
wanafunzi zaidi ya nusu waliochaguliwa kwenda sekondari ni wale wa
daraja la D, hapo kuna kazi kubwa sana, tunaweza kuwa na mbumbubu wengi
Sekondari kwahiyo nashauri Serikali iandae walau mpango wa wiki mbili
kabla ya shule kufunguliwa ili kuwasaidia hawa watoto,”alisema.
Lyimo
alisema ofisi yake itaendelea kufanya utafiti ili kubaini sababu za
kufanya vibaya kwa wanafunzi katika mtihani huo na kwamba itatoa taarifa
baada ya kupata matokeo ya kitaalamu kuhusu suala hilo.
CHANZO:MWANANCHI GAZETI
No comments:
Post a Comment