Tuesday, October 16, 2012

ZANZIBAR YAFANYA MABADILIKO YA BARAZA LA MAWAZIRI



 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt Ali Mohammed Shein amefanya mabadiliko katika Baraza la Mapinduzi.

 Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi,Dkt Abdulhamid Yahya Mzee imesema katika mabadiliko hayo, Rais Dkt Shein amemteua Shawana Bukheti Hassan kuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Rais Dkt Shein amefuta uteuzi wa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi,Mansoor Yussuf Himid. 

Katika uteuzi mwengine Dkt Shein amewateua Mtumwa Kheir Mbarak kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili na Mohammed Said Mohamed kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Katika hatua nyengine, Rais Dkt Shein amefanya mabadiliko ya baadhi ya Makatibu Wakuu katika Wizara za Miundombinu na Mawasiliano, Wizara ya Ardhi,Makaazi,Maji na Nishati.

 Dkt. Juma Malik Akili ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano akichukua nafasi ya Dkt. Vuai Idd Lila atapangiwa kazi nyengine. Ali Khalil Mirza ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Ardhi,Makaazi,Maji na Nishati. 

Kabla ya uteuzi huo, Mirza alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar,aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Mwalimu Ali Mwalimu atapangiwa kazi nyengine. Taarifa ya Ikulu imesema pia Rais Dkt Shein amemteua Tahir M. Abdulla kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano,aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Msanif Haji Mussa atapangiwa kazi nyengine. 

Uteuzi mwengine ni Mustafa Aboud Jumbe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,Makaazi,Maji na Nishati. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alikuwa Tahir M Abdulla ambaye amehamishiwa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano. 

Rais Dkt Shein ameteua CDR Julius Nalim Maziku kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kapteni Juma Abdulla Juma ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar hivi karibuni. 

Uteuzi mwengine ni Juma Ameir Hafidh ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais(Fedha,Uchumi na Mipango ya Maendeleo) ambaye amechukuwa nafasi iliyoachwa wazi na Abdi Khamis Faki aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar. 

Aidha, aliyepata kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz ameteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar ambaye anachukuwa nafasi iliyoachwa wazi na Ali Khalil Mirza aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi,Maji na Nishati. 

 Pia Rais Dk Shein amemteua Mussa Haji Ali kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu uchumi Zanzibar. Uteuzi huo wote unaanza Oktoba 15 mwaka 2012. 

         Imetolewa na: Idara ya Habari(MAELEZO) Zanzíbar leo tarehe 15/10/2012

No comments:

Post a Comment