TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI UFAFANUZI KUHUSU SISI KUJIUNGA NA CHADEMA NA MALUMBANO KUHUSU MAJINA YETU
Tarehe 30/09/2012 mimi Esther Wasira na dada yangu Lilian Wasira tulijiunga na CHADEMA na kukabidhiwa kadi na Katibu Mkuu wa CHADEMA Mh. Dr Willibrod Slaa. Tulielezea kwa kirefu sababu za sisi kujiunga CHADEMA na tukasisitiza kuwa tumeridhika kuwa CHADEMA ni chama chenye dhamira safi ya kuiongoza Tanzania na kwamba ni chama kinacholeta matumaini mapya ya kuijenga Tanzania mpya yenye neema. Waandishi wa habari walijaribu sana kutudodosa kujua tuna uhusiano gani na Waziri Steven Wasira.
Tulielezea wazi kuwa mahusiano yetu ya kifamilia hayahusiki na sababu na dhamira yetu ya kujiunga CHADEMA. Hata hivyo tulielezea kuwa Waziri Steven Wasira ni baba yetu mdogo ambaye alinyang'anyana ziwa na baba yetu mzazi, wakili George Wasira. Tulidhani hiyo ilitosha na lisingekuwa swala tena la kujadili na badala yake hoja ya kujadiliwa ingeweza kuwa sababu tulizozieleza za kujiunga CHADEMA. Tunasikitishwa sana na malumbano yaliyofuata baada ya hapo kuhusu kama sisi ni watoto wa Wasira au la.
Kama tulivyoeleza, tumejiunga CHADEMA kwa sababu tulizozieleza hapo awali na wala si kwa sababu nyingine yeyote. Hatujajiunga CHADEMA kumdhalilisha mtu, kumfedhehesha mtu au kukipatia umaarufu CHADEMA kwa vile tu tunatumia jina la Wasira.
CHADEMA ni chama cha siasa tena chenye wanachama na wafuasi wengi Tanzania hivyo si kashfa bali ni fahari kubwa mtu kujiunga CHADEMA na tena ni ushahidi wa mtu kujitambua. Pia CHADEMA ni Chama maarufu sana Tanzania kwa sasa hata pengine ni maarufu kuliko CCM hivyo hakihitaji kujipatia umaarufu kwa mgongo wetu. Sisi tunawaheshimu sana wazee wetu na tutaendelea kuwaheshimu ila linapokuja swala la chama cha kujiunga linabaki kuwa hiari yetu kwa kuzingatia sera za chama na uwezo wa chama husika katika kujenga Tanzania tunayoitaka na hilo ndilo lililotupeleka CHADEMA. Na hii ni haki yetu ya msingi kabisa inayolindwa na Katiba ya nchi hii chini ya ibara ya 20(1).
Ikumbukwe kuwa mmoja wa Waanzilishi wa CHADEMA ni Mzee Wasira. Dhamira ya kuanzisha CHADEMA ilikuwa ni kushika dola na hili ndilo CHADEMA imekuwa siku zote inajaribu kuwashawishi Watanzania kuwa sasa wamekomaa na wanastahili kuchukua dola. Kwa vile kuchukua dola ilikuwa ndio ndoto ya baba yetu mzazi Mwanzilishi wa CHADEMA, sisi kama watoto tumejiunga na M4C ya CHADEMA ili tuweze kutimiza ndoto ya baba yetu kuwa CHADEMA siku moja ichukue jukumu la kuiongoza Tanzania.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na: Lilian Wasira 0719 604156 Esther Wasira 0655 048797
No comments:
Post a Comment