ROONEY atimiza Goli 200 kwa Klabu, RIO amkera FERGIE!
Jumapili, 21 Oktoba 2012 11:44
JANA OLD TRAFFORD, ambako Manchester United waliitwanga Stoke City Mabao 4-2 katika Mechi ya Ligi Kuu England, Wayne Rooney alifikisha Mabao 200 kwa kufungia Klabu, Man United na Everton, lakini pia uamuzi wa Beki Rio Ferdinand kutovaa Fulana ya Kampeni za Ubaguzi, ‘KICK IT OUT’, wakati wa kupasha moto kabla ya Mechi hiyo umemtibua Meneja wake Sir Alex Ferguson.
Katika Mechi hiyo ya jana, Rooney alifunga Bao 3, moja akijifunga mwenyewe na kuipa Stoke City uongozi wa bao 1-0, lakini alijirekebisha na kusawazisha na kisha, baadae, kuipigia Man United bao jingine ambalo liliipa Man United ushindi wa bao 4-2 huku bao nyingine mbili zikifungwa na Robin van Persie na Danny Welbeck.
Kwa kujifunga mwenyewe na kisha kuifungia Man United mabao katika Mechi moja, Wayne Rooney amekuwa Mchezaji wa kwanza wa Man United kufanya hivyo tangu David Beckham alipokumbwa na mkasa kama huo Mwaka 2001.
Wakati Rooney akifanya miujiza yake, Man United imekumbwa na mvutano kati ya Meneja wao Sir Alex Ferguson na Mchezaji wake Rio Ferdinand kuhusu kuisapoti Kampeni ya kupinga Ubaguzi wakati ambao Wiki hii Kampeni ya ‘KICK IT OUT’ ndio imeshamiri na Wachezaji kuombwa kuvaa Tisheti zenye maandishi hayo ili kupinga Ubaguzi.
Majuzi Ijumaa, Ferguson alitamka kuwa Mchezaji wa Reading Jason Roberts amepotoka baada ya kutamka waziwazi hatavaa Tisheti hizo ikiwa ni kuonyesha kukerwa kwake na usimamizi duni wa kupinga ubaguzi na hasa kumuona John Terry, ambae alipatikana na hatia ya kumkashifu Kibaguzi Mdogo wake Rio Ferdinand, Anton Ferdinand, kupewa adhabu hafifu ya kufungiwa Mechi 4 na Faini ya Pauni 220,00 wakati Straika wa Liverpool Luis Suarez alifungiwa Mechi 8.
Sir Alex Ferguson amesema watalishughulikia suala la Rio Ferdinand kugoma kuvaa Tisheti hizo ndani ya Klabu.
Akiongea mara baada kuifunga Stoke City bao 4-2, Ferguson alisema: “Nimehuzunishwa. Nilisema jana Wachezaji wavae Fulana hizo ili kuiunga PFA [Professional Footballers' Association] na kila Mchezaji afuate. Sasa yeye katuangusha. Tutalishughulikia suala hili, usiwe na wasiwasi!”
Baadae Ferguson akaongeza: “Niliongea na Wanahabari kuhusu hili. Imenifedhehesha.”
Hata hivyo, baadhi ya Wadau wameibuka kuunga mkono uamuzi wa Rio Ferdinand wakidai uamuzi huo ni wa Mtu binafsi katika kitu anachokiamini.
Akiongea na RADIO 5, Mchezaji wa zamani wa Wales aliewahi kuichezea Man United, Robbie Savage, amesema: “Ninaheshimu misimamo ya Jason Roberts na Rio Ferdinand. Ukifikiria zaidi utashangazwa na alichokisema Ferguson. Anasema amefedheheshwa. Hili si suala lake. Fergie ni Meneja Bora kupita wote katika historia lakini ni uamuzi binafsi wa Rio kuvaa au kutovaa Tisheti ile!”
No comments:
Post a Comment