Friday, October 19, 2012

MTANZANIA KUCHEZA MPIRA MAREKANI

Mchezaji Millan Mbise kutoka Tanzania ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) itakayomwezesha kucheza mpira wa miguu nchini Marekani.
 
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Marekani (USSF) limemuombea hati hiyo Mbise kama mchezaji wa ridhaa ili ajiunge na timu ya Virginia Youth Soccer.
 
Klabu ya zamani ya Mbise aliyezaliwa Agosti 18, 1994 imetajwa kuwa Super Sport FC, na mechi ya mwisho kwenye timu hiyo alicheza Novemba 15 mwaka juzi.
 
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanya mawasiliano na pande husika kabla ya kutoa hati hiyo kwa mchezaji huyo kama ilivyoombwa na shirikisho hilo la Marekani.
 
TASMA WAANZA MCHAKATO WA UCHAGUZI
Chama cha Madaktari wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) leo (Oktoba 19 mwaka huu) kimetangaza kuanza mchakato wa uchaguzi wa chama hicho uliopangwa kufanyika Novemba 28 mwaka huu.
 
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dk. Francis Mchomvu, fomu kwa wanamichezo wanaotaka kugombea uongozi wa chama hicho zitaanza kutolewa Oktoba 21 mwaka huu.
 
Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu hizo zinazopatikana ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni saa 10.00 alasiri ya Oktoba 26 mwaka huu. Ada ya fomu kwa nafasi nne za juu ni sh. 200,000 wakati kwa nafasi nyingine zilizobaki ni sh. 100,000. Kati ya Oktoba 27-31 mwaka huu Kamati ya Uchaguzi ya TASMA itapitia fomu na kutangaza majina ya waliojitokeza kuomba uongozi.
 
Nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mhazini, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji.
 
Kipindi cha pingamizi kwa waombaji ni kuanzia Novemba 1-6 mwaka huu, na pingamizi zinatakiwa kuwasilishwa kwa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 6 mwaka huu. Hakuna ada kwenye pingamizi.
 
Pingamizi zitajadiliwa na kufanyiwa uamuzi kati ya Novemba 7-9 mwaka huu. Usaili utafanyika kati ya Novemba 10-11 mwaka huu ambapo matokeo ya usaili huo vilevile yatatangazwa ili kutoa fursa kwa rufani ambazo zinatakiwa kukatwa kati ya Novemba 11-13 mwaka huu.
 
Rufani ambazo zinaambatana na ada y ash. 500,000 zinatakiwa kufikishwa kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 13 mwaka huu.
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment