Wednesday, October 17, 2012

MPONDA AMTISHA KIKWETE

JUMUIYA na Taasisi za Kiislamu nchini, zimeipa serikali siku saba kuwapa dhamana watuhumiwa wa Kiislamu wanaoshikiliwa kutokana na vurugu zilizotokea hivi karibuni maeneo ya Mbagala, jijini Dar es Salaam, na kusababisha makanisa kuchomwa moto na kuharibu mali nyingine kadhaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika hoteli ya Lamada, Katibu wa Jumiya hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda, alisema Waislam hao wanapaswa kupewa dhamana kwa kuwa ni haki yao kisheria.
Ponda alisema endapo siku hizo zitaisha bila kupewa haki hiyo watatangaza nini watakifanya ili kuondoa ukandamizaji huo.

Alisema katika vurugu zile waliokamatwa wengi ni Waislamu huku hoja ya kuwanyima dhamana ikiwa ni suala la kuharibiwa makanisa ambayo imechukuliwa kuwa ni ya kitaifa.
Tabia hiyo ya viongozi wa serikali kuyafanya mambo ya kanisa kuwa ya kitaifa na kudharau Waislamu na haki zao, Sheikh Ponda alisema ndiko kunakochangia kuligawa taifa katika misingi ya udini.

Sambamba na hilo pia waliitaka serikali kutoa tamko rasmi la kulaani kukojolea Kuran na kuongeza kwamba lile alilolitoa Rais Jakaya Kikwete katika kilele cha mbio za Mwenge hawalitambui na wala halitoshi kutokana na ukubwa wa tukio lenyewe.
Wasikitishwa JK kutotembelea misikiti
Jumuiya hiyo pia imesikitishwa na kitendo cha Rais kwenda kutembelea makanisa tu wakati vurugu hizo pia zilisababisha baadhi ya misikiti kuchomewa makapeti kwa mabomu yaliyokuwa yanarushwa na Jeshi la Polisi na watu kujeruhiwa.
“Rais alipofanya ziara katika kanisa la Zakiem alipita mita tatu jirani na msikiti wa Hijra ambapo makapeti yake mpaka tunakwenda mitamboni yameloa damu kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na polisi waliokuwa wakilinda doria katika kanisa hilo, alisema.

Waislamu hawajahusika na uvunjaji wa makanisa
Katika hatua nyingine Sheikh Ponda alisema Waislam hawajahusika na uvunjwaji wala uchomaji wa makanisa na kueleza vurugu zilitokea siku ambayo Waislam walikusanyika kwa wingi katika msikiti maalum kwa ajili ya ibada ya sala ya Ijumaa.

Alisema polisi walikuwa na upande katika tukio hilo kwani misikiti ya Ijumaa ilianza kuzingirwa mapema kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi na ilipofika majira ya saa 6:00 mchana baadhi ya misikiti ikiwemo ile iliyoko umbali wa kilometa mbili kutoka kituo cha polisi Maturubai, ilianza kushambuliwa kwa mabomu.
Wakati wa mashambulizi hayo, Ponda anadai makanisa yalionekana kupewa ulinzi wa amani huku misikiti ikipelekewa vikosi vya kushambuliwa.
Hata hivyo ilipotimu majira ya saa 9:00 alasiri alidai alifika mmoja wa maafisa kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambaye aliwahoji masheikh waliokuwepo eneo la Maturabai na kutaka kujua ni kwa nini hawashiriki katika kusaidia kutuliza vurugu zinazoendelea kati ya polisi na Waislamu.

Baada ya kuwepo kwa mvutano wa muda mrefu kati ya Kamanda wa Polisi wa Temeke, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Maturubai, masheikh hao na Waislamu waliofika kituo cha polisi cha Maturabai ili kushinikiza kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa aliyekojelea Kuran, muafaka ulikuwa ni masheikh kwenda viwanja vya Zakiem kwa lengo la kuwatuliza waumini wao.

Huku pendekezo la pili likiwa ni la Waislam wote waliokamatwa watolewe mahabusu na la tatu ni polisi kutoa gari na vipaza sauti kwa masheikh ambapo hilo la kuzungumza na waumini lilikamilika kwa msaada wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambao walitoa msaada wa gari kwa masheikh.

“Kilichotokea baada ya masheikh kuondoka na waumini walijikuta wakishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya vurugu ambapo polisi walimwagwa mitaani na kuwakamata watu wasiokuwa na hatia, ukamataji uliohusisha kuhojiwa watu majina, kuandamwa kwa mbio mtu aliyevaa kanzu, kofia na kuachwa aliyevaa msalaba akikatiza katikati ya askari na hatimaye matumizi ya nguvu kubwa kwa aliyekamatwa.

“Hatua hii ndiyo iliyopelekea kukamatwa kwa watuhumiwa wengi waliokuwa mikononi mwa polisi mpaka leo na ndiyo iliyochochea vurugu zilizosambaa mitaani,” alisema Sheikh Ponda.
Maaskofu wakutana, watafakari
Baraza la Maaskofu nchini limewataka Wakristo kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kwani viongozi wao bado wanajadili suala hilo la kuchomewa makanisa na kuona ni hatua gani wataweza kuzichukua.

Katibu wa Baraza hilo, Antony Makunde, alisema pia wanapaswa kulinda nyumba zao za ibada na kujumuika kwa pamoja kufanya maombi kwa pamoja kwa kuwa usalama na ulinzi wa maisha yao uko mikononi mwa Mungu.
Hata hivyo walisifu juhudi ambazo zimefanywa na polisi katika kutuliza vurugu hizo na kuongeza kwamba wametembelea makanisa yaliyoathirika na kujionea hali halisi ambayo inasikitisha.
Padri Makunde alisema haiwaangii akilini kuwa Watanzania wamefikia hatua hiyo ya kushindwa kuvumiliana na kupongeza hatua ya Wakristo kutojibizana katika tukio lile kwani lingeleta madhara zaidi.

Chanzo cha vurugu

Chanzo cha vurugu hizo ni ubishani wa kitoto uliozuka baina ya mtoto Emmanuel na mwenzake Zakaria Hamis (12) anayesoma Shule ya Msingi Chamazi, Jumatano ya wiki iliyopita.
Inadaiwa kwamba Zakaria alimwambia Emmanuel ambaye pia ni jirani yake, kwamba Msahafu huo ni mtakatifu na kwamba mtu yeyote ambaye angeuharibu kwa jambo lolote, iwe ni kuuchana kwa makusudi, kuutemea mate au kuukojolea angekufa palepale au kugeuka mjusi.

Katika ubishi huo, Emmanuel aliamua kuukojolea msahafu huo, akitaka kuona kama kweli angekufa au kudhurika, jambo ambalo halikumpendeza rafiki yake ambaye alikwenda kuwaeleza wazazi wake ambao walikwenda polisi kuyamaliza.

Kabla jambo hilo halijamalizwa ndipo
 vurugu zilipozuka siku ya Ijumaa na kusababisha makanisa takriban saba kuharibiwa kwa kuyachomwa moto na kuibiwa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya mamilioni ya fedha.
Watu 37 wakiwemo wanawake wawili wanaotuhumiwa kuchoma makanisa, kufanya uharibu wa mali na kuiba kwa kutumia nguvu huko Mbagala Zakhem, jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali.

Naye mtoto aliyesababisha vurugu hizo ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Chamazi-Machimbo Mbagala, alifikishwa katika mahakama ya watoto mbele ya Hakimu Mkazi Devota Kisoka akikabiliwa na kosa moja la kuidhalilisha dini ya Kiislamu kwa kuikojolea Koran, Oktoba 10.

Washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo wakiwa kwenye magari matatu ya polisi aina ya Defender majira ya saa 6:26 mchana chini ya ulinzi mkali wa askari waliokuwa wamevalia mabomu viunoni.
Baada ya kushushwa, watuhumiwa hao waliamriwa kuchutama kabla ya kuanza kuingizwa kwenye chumba namba moja cha mahakama hapo huku kukiwa na tahadhari kubwa ya kiusalama ndani na nje ya mahakama hiyo.

Kwa upande wa mashtaka, watuhumiwa hao wamefunguliwa kesi nne tofauti za jinai kwa mpigo, kesi ya kwanza ni jinai Na.240/2012. 241/2012,242/2012 na 243/2012.
Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka hayo mbele ya Mahakimu Wakazi wawili Sundi Fimbo anayesikiliza kesi tatu huku moja ikisikilizwa na Hakimu Mkazi Bingi Mashabara.
Upande wa jamhuri kwenye keshi hiyo uliwakilishwa na Wakili Mwandamizi Tumaini Kweka, Lasdlaus Komanya na Joseph Maugo.

Wakili Kweka alidai katika kesi ya jinai namba 243/2012 inayowakabili washtakiwa 17 ambao ni Maenga Rwenda, Hamad Euli, Shego Sheso, Ramadhan Mgule, Mashaka Iman, Kassim Juma Kigoni, Ibrahim Himu, Hamza Fundi Hamza, Mikidadi Sadick, Juma Mbegu, Rahimu Boga, Issa Abdallah, Hamis Kmwaga, Ramadhan Mbulu, Hamed Mohamed, Mohamed Yusuf na Msha Alifa ambao wanakabiliwa na kosa la kula njama kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287A cha sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2012.

Wakili Kweka alidai kuwa Oktoba 12, mwaka huu, huko Mbagala watajwa waliiba vitu mbalimbali ikiwemo laptop, printer projector, spika, saa za ukutani, viti vya plastiki vyote vikiwa na thamani ya sh 20, 000,000 mali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Usharika wa Mbagala.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa kabla ya kuiba watuhumi
wa walimtishia mlinzi, Michael Samwel, kwa mashoka na nondo kwa lengo la kujipatia vitu hivyo.

Kweka alidai shtaka jingini ni la kuchoma kanisa kinyume na kifungu cha 319(a) cha sheria ya Kanuni ya Adhabu ambapo washtakiwa hao kwa nia ovu walichoma kanisa hilo na mali na kuongeza kuwa shtaka jingine ni la kuharibu mali kama madirisha, meza, mfumo wa umeme, milango, ‘air conditioner’ vyote mali ya kanisa hilo ambavyo vyote vikiwa na thamani ya sh 500,000,000.

Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashtaka hayo na wakili Kweka akadai shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha, halina dhamana isipokuwa yaliyosalia, hivyo Hakimu Fimbo na mwenzake Mashabara, waliahirisha kesi zote hadi Oktoba 30.

Hiyo ikafanya washtakiwa wote 37 wanaokabiliwa na makosa yenye dhamana na lisilowezekana kupewa dhamana, kurejea mahabusu, hivyo ndugu, jamaa na marafiki kuangua vilio nje ya viwanja vya mahakama hiyo.

Aidha katika kesi namba 242/2012 inayomkabili Hashimu Ligongo (30) na wenzake 10, wanakabiliwa na makosa ya wizi wa redio ya gari namba T813 AAw Toyota Corona yenye thamani ya sh 300,000 mali ya Nocholaus Mitamba.

Makosa mengine kwa washtakiwa hao ni wizi wa ‘power window’ kwenye gari namba T.180 AYM Suzuki Escudo mali ya Melkior Rweyemamu. Kosa jingine ni kuharibu gari la polisi aina ya Land Lover lenye namba za usajili PT 2068 ambapo uharibifu wake ni wa thamani ya sh 2,000,000 na wizi wa vitu mbalimbali mali ya kanisa la S.D.A zenye thamani ya sh. mil. 8.47.

Aidha, wakili Joseph Mahugo alidai shtaka jingine ni uharibifu wenye thamani ya shilingi mil. 1.5 wa gari la Puma mali ya seriakali, pia kuchoma na kuiba katika makanisa ya Anglicana, Tanzania Assemblies of God huko Mbagala.

Baada ya mawakili wa serikali kuwasomea mashtaka hayo, waliomba mahakama itoe dhamana kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 148(5)(e) cha sheria ya makosa ya jinai katika kesi tatu namba 240/2012. 241/2012 na 242/2012 ambazo makosa yake yana dhamana na upelelezi haujakamilika.
Hakimu kwa upande wao, walisema kweli kesi hizo tatu zina dhamana isipokuwa kesi namba 143/2012, lakini kwa jana hawakuwa tayari kusikiliza maombi ya dhamana hadi Oktoba 30.
   KUTOKA TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment